Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kinachofanyika jijini Harare, Zimbabwe Machi 6-7, 2025.
Kikao hicho ambacho ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa SADC unaotarajiwa kufanyika jijini hapa tarehe 12 Machi 2025, kimepokea na kujadili taarifa mbalimbali ambazo zimewasilishwa kwao na Kamati ya Wataalam.
Taarifa zilizojadiliwa katika Mkutano huo ni pamoja na Tathmini ya utekelezaji wa Maamuzi ya Mikutano iliyopita ikiwemo ya Baraza la Mawaziri na ile ya Wakuu wa Nchi na Serikali; Taarifa kuhusu Mpango wa Bajeti kwa mwaka wa Fedha 2025/2026; Mapitio ya Sera na Itifaki mbalimbali za Jumuiya ya SADC; na Mapitio ya utekelezaji wa Mpango Mkakati Elekezi wa Maendeleo wa Kanda (RISDP) 2020-2030 hususan katika nguzo kuu nne za vipaumbele pamoja na maeneo mtambuka.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Balozi Mussa ametoa rai kwa Nchi Wanachama wa SADC kuendelea kutekeleza maamuzi yanayofikiwa kwenye vikao mbalimbali hususan yale yanayohitaji hatua za moja kwa moja za nchi wanachama ili kuziwezesha nchi hizo kufikia malengo yaliyowekwa kwa maendeleo endelevu ya Kanda.
Pia alisisitiza umuhimu wa Nchi zote Wanachama kuwekeza katika kufanya tathmini na ufuatiliaji ya utekelezaji wa maamuzi hayo.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo, Mwenyekiti ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara za Kimataifa wa Zimbabwe, Balozi Albert Chimbindi pamoja na kuwasisitiza wajumbe kujadili taarifa hizo kwa kina, pia amesema anatiwa moyo na ari iliyopo kwa nchi wanachama katika kuhakikisha malengo ya kuanzishwa kwa Jumuiya ya SADC yanafikiwa ikiwemo maendeleo ya kiuchumi na amani na usalama.