FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ali Mussa, amewataka wahasibu nchini kuwa na uadilifu wakati wa kutekeleza majukumu yao, bila ya kufanya upendeleo wa aina yoyote.
Dkt. Mussa ametoa kauli hiyo alipokuwa akifungua Kikao cha Pili cha Baraza la Tano la Wafanyakazi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kilichofanyika mjini Morogoro, ambapo amewahimiza wafanyakazi kuwajibika ipasavyo, kuheshimu muda wa kazi, na kuzingatia weledi ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima sehemu za kazi.
Aidha, aliiomba TIA kuendelea kuanzisha programu mpya za masomo ili kuendana na mabadiliko ya wakati, huku akisisitiza matumizi ya mifumo ya masomo kwa njia ya mtandao (online learning).
Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Profesa William Amos Pallangyo, amesema kuwa baraza hilo linatoa fursa kwa wafanyakazi kujadili taarifa za utendaji, changamoto zilizopo, na mapendekezo ya kuzitatua. Kikao hicho kilijumuisha mjadala wa bajeti ya taasisi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na taarifa za fedha na ukaguzi.
Profesa Pallangyo ameeleza kuwa TIA tayari imepata kibali cha kuanzisha kozi za mtandaoni (online learning), na utekelezaji wake utaanza hivi karibuni.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi, Margreth Mwamasso, akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa baraza hilo ameema kuwa wataendelea kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kujiendeleza kielimu ili kufuata mabadiliko ya teknolojia ya kisasa. Alisisitiza pia umuhimu wa uwajibikaji kwa wafanyakazi wote ili kuongeza tija katika taasisi na kwa mtu binafsi.