Mwenyekiti wa Tume, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, akizungumza kuhusu zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, mkoa wa Dar es Salaam kwenye ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.
……………..
Na. Mwandishi Wetu
Dar es Salaam – Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza mpango wa kuandikisha wapiga kura wapya 643,420 jijini Dar es Salaam kati ya Machi 17 na 23, 2025. Hata hivyo, wadau wa uchaguzi wameanza kuhoji ufanisi wa zoezi hilo, wakitaka uhakika wa usimamizi mzuri na uwazi wa mchakato huo.
Akizungumza leo Machi 5, 2025, Mwenyekiti wa Tume, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, amesema uandikishaji huo ni sehemu ya awamu ya kwanza ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ambalo limekwisha kufanyika katika mikoa 28 nchini.
“Tume inatarajia baada ya uandikishaji, Mkoa wa Dar es Salaam utakuwa na wapiga kura 4,071,337, lakini idadi hii inaweza kuongezeka endapo wapo waliostahili kujiandikisha lakini hawakufanya hivyo mwaka 2019/20,” alisema Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Ramadhan.
Licha ya mipango hiyo, baadhi ya wadau wameeleza mashaka juu ya muda mfupi wa zoezi hilo, wakisema siku saba pekee huenda zisitoshe kuhakikisha kila mwenye sifa anapata nafasi ya kujiandikisha. Aidha, swali limeibuka kuhusu ufanisi wa vituo 1,757 vilivyotengwa, ikizingatiwa kuwa ni ongezeko dogo la vituo 96 tu ikilinganishwa na mwaka 2019/20.
“Tuna wasiwasi na maandalizi haya, hasa kwa idadi kubwa ya watu Dar es Salaam. Je, vifaa vya kutosha vipo? Je, watumishi wa Tume wako tayari kuhakikisha kila mwenye haki anajiandikisha bila changamoto?” amehoji mdau mmoja wa uchaguzi ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Pamoja na hilo, Tume imetangaza kuwa itatoa nafasi kwa waliopoteza kadi zao, waliohama maeneo yao, na wale wanaotaka kurekebisha taarifa zao. Hata hivyo, bado haijaweka wazi mikakati madhubuti ya kuhakikisha kila hatua inatekelezwa kwa uwazi na bila upendeleo.
Je, Tume itaweza kusimamia zoezi hili kwa ufanisi na kuhakikisha kila mwenye haki anajiandikisha bila vikwazo? Wadau wa uchaguzi na wananchi wanaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo yake.
Akiwasilisha mada kwenye mkutano huo, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ndugu. Kailima Ramadhan amefafanua kuwa kwa mkoa wa Dar es Salaam Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 643,420 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 18.7 ya wapiga kura 3,427,917 waliopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
“Tume inatarajia baada ya uandikishaji Mkoa wa Dar es Salaam utakuwa na wapiga kura 4,071,337. Aidha, idadi hii inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana wapo watanzania ambao walikuwa na sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wakati wa uboreshaji wa Daftari mwaka 2019/20, lakini kwa sababu moja au nyingine hawakuweza kujiandikisha,” amesema Kailima.
Ameongeza kuwa mkoa wa Dar es Salaam una vituo 1,757 vitakavyotumika kwenye uboreshaji kwa mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo 96 katika vituo 1,661 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka 2019/20.
Kailima amesema zoezi la uboreshaji wa Daftari linahusu kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi na watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, kutoa kadi mpya kwa wapiga kura waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika na kutoa fursa kwa wapiga kura walioandikishwa kurekebisha taarifa zao yakiwemo majina na taarifa nyingine.