*Watanzania kujengewa uwezo kwenye teknolojia ya uchimbaji na uchenjuaji madini
*Vyuo vya VETA kutumika kutoa mafunzo maalum
*Canada yaipongeza Tanzania kwa kukuza sekta ya madini
*Mpango wa Uwezeshwaji wa Vijana na wakina mama waungwa mkono
𝐓𝐨𝐫𝐨𝐧𝐭𝐨,𝐂𝐚𝐧𝐚𝐝𝐚
Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada Mh. Ahmed Hussein na Waziri wa Madini wa Tanzania Mh. Anthony Mavunde wamefanya mazungumzo ya masuala mbalimbali ya kuboresha uhusiano baina ya nchi mbili hizo hasa katika eneo la kuwajengea uwezo wataalamu na wachimbaji wa madini nchini Tanzania katika matumizi ya teknolojia ya kisasa ya uchimbaji na uchenjuaji madini.
Mazungumzo hayo yamefanyika jana Toronto,Canada na kuhudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Canada Mh. Joseph Sokoine sambamba na wataalamu wa Wizara zote mbili.
Akitoa maelezo ya awali, Waziri Ahmed Hussein ameipongeza Tanzania chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa namba ambayo imeweka mazingira mazuri ya ukuaji wa sekta ya Madini nchini na kwamba Canada itaendelea kuimarisha uhusiano wake na Tanzania hasa katika eneo la kuwajengea uwezo wataalamu na wachimbaji madini kwenye matumizi sahihi ya teknolojia ya uchimbaji na uchenjuaji madini.
“Tumekuwa na miradi ya maendeleo ya elimu nchini Tamzania,hivyo kupitia vyuo vya mafunzo ya Ufundi itakuwa rahisi kuja na mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wananchi wa Tanzania,hasa wakina mama na vijana, kushiriki kikamilifu kwenye mnyororo mzima wa sekta ya madini“Alisema Hussein
Kwa upande wake, Waziri Anthony Mavunde ameishukuru nchi ya Canada kwa ushirikiano mkubwa inaoutoa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania na pia kubainisha uwepo wa Kampuni kubwa za Madini kutokea nchini Canada zimechochea kwa kiwango kikubwa maendeleo ya kiuchumi kupitia fursa mbalimbali zitokanazo na uwekezaji huo.
“Tanzania hivi sasa tuna programu yenye lengo la kuwezesha ushiriki kamilifu wa wakinamama na Vijana kwenye sekta ya madini,hivyo kuwajengea uwezo wa kiujuzi kwenye mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya madini kutachochea kukua kwa kasi kwa sekta ya madini.
Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi vinaweza kutumika kutoa mafunzo maalum ya jamii husika kutokana na aina ya shughuli za madini katika eneo husika.
Tanzania itatoa ushirikiano wa kutosha kwa Canada katika utelekezaji wa mpango huu wenye tija kwa nguvu kazi ya Taifa Tanzania.“Alisema Mavunde
Akitoa maelezo ya ziada,Balozi Joseph Sokoine ameikaribisha mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini Canada kuwekeza nchini Tanzania kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la ujenzi wa miundombinu na kwenye sekta ya madini.