Mwamvua Mwinyi, Chalinze Februari 5, 2025
Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne na Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Salma Kikwete, amekemea vitendo vya baadhi ya watoto wa kiume kujibadili na kuwa na tabia za kike na kuomba wazazi kusema na watoto .
Aidha, ametoa rai kwa wasichana na wanawake kujikita katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi ujao bila kuwa na woga.
Akizungumza katika kongamano la Siku ya Wanawake Duniani lililofanyika Halmashauri ya Chalinze, mkoani Pwani, Salma alisisitiza kuwa jamii inapaswa kuzingatia malezi bora, kwani bila ya malezi bora, hatuwezi kuwa na taifa bora.
Alisisitiza pia umuhimu wa watoto kupata elimu, hususan elimu ya dini, ili kuwajenga kiimani.
“Miaka ya nyuma, mtoto alipotenda mambo kinyume na maadili, mtu yeyote alikuwa na haki ya kumkosoa, ‘mtoto wa mwenzio ni mtoto wako.’ lakini sasa hali imekuwa tofauti,” alisema Salma.
Alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusimamia suala la malezi na makuzi ya watoto, pamoja na kuimarisha haki kwa wanawake na kupigania usawa wa jinsia.
Salma alisisitiza kwamba watoto wa kike wanapaswa kusimamia elimu yao na wasikubali kudanganywa au kukatisha ndoto zao.
Kuhusu uchaguzi ujao, alisisitiza kuwa wanawake mwaka huu wana nafasi yao, na kwamba wanampa Rais Samia kura si kwa sababu ni mwanamke, bali kwa sababu ni kiongozi mwenye uwezo na Rais mwanamke wa kwanza barani Afrika.
“Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi, na mategemeo ni kuongeza idadi ya wabunge na madiwani ili kuongeza nafasi ya wanawake kwenye ngazi za maamuzi,” alisisitiza Salma.
Awali, Asia Festus, Wakili na Mratibu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, pamoja na maofisa wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika Halmashauri ya Chalinze, alieleza kuwa wakiwa Chalinze walitoa ushauri wa sheria kwa kata kumi na vitongoji 30 kwa siku tisa.
Asia alifafanua kuwa kampeni hiyo, iliyoendeshwa kuanzia Februari 25 hadi Machi 5, 2025, mkoani Pwani, ililenga kutoa elimu kuhusu masuala ya kisheria, utatuzi wa migogoro, na ushauri wa kisheria huku Pwani ilikuwa ni mkoa wa 20 kunufaika na huduma hii.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Zainab Vullu, alisema Rais Samia Suluhu Hassan alishiriki Mkutano wa Beijing akiwa na miaka 30, na leo hii anakwenda kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha Siku ya Wanawake Duniani, akiwa Rais mwanamke wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Wapo baadhi ya watu walimbeza na kumkejeli kuwa hatoweza kuendeleza nchi, lakini leo hii amekuwa mfano wa kuigwa kwa utawala bora na kuimarisha uchumi kupitia mafungu ya fedha za mikopo kwa wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu,” alisema Vullu.
Alisema mkoa wa Pwani una deni la kumlipa Rais Samia kwa juhudi zake za kuinua maendeleo mkoani humo.
Mbunge wa viti maalum mkoani Pwani, Subira Mgalu, alieleza kuwa Tanzania imepata Rais mwanademosia ambaye ni kiongozi anayethamini mfumo wa vyama vingi na ameweka mazingira wezeshi kwa maendeleo ya kisiasa.
Agnes Hanti, Mratibu wa Mradi wa Kuwezesha Wanawake katika Uongozi na Haki za Kiuchumi (WLER), akizungumza kwa niaba ya Mwakilishi Mkazi wa UN Women Tanzania, bi. Hodan Addou, alisisitiza, uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake ni hatua muhimu zaidi na yenye ufanisi katika kufikia usawa wa kijinsia.
“Tunaposheherekea Siku ya Wanawake Duniani na kutafakari kuhusu ajenda ya Beijing+30, tuzingatie kuwa kukuza uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake si ndoto ya mbali, bali ni lengo la vitendo linalohitaji hatua thabiti katika ngazi zote,” alieleza Hanti.