Rais wa Baraza la Taifa na Bunge la Jamhuri ya Cuba, Mhe. Esteban Lazo Hernandez, amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam Mhe. Hernandez amepokelewa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Ndriananga na Balozi wa Tanzania nchini Cuba Mhe. Hamphrey Polepole.
Ziara ya Mhe. Esteban Lazo Hernandez nchini inalenga kuendelea kuimarisha na kuendeleza ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba.
Akiwa nchini Mhe. Hernandez atakutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb.), Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zanzibar, Mhe. Zubeir Ali Maulid, Mjane wa Baba wa Taifa hayati Mwl. Nyerere Mama Maria Nyerere.
Vilevile, atatembelea Makumbusho ndogo ya Mwl. Nyerere iliyopo jijini Dar es Salaam na Kiwanda cha uzalishaji wa viwatilifu hai cha Tanzania Biotech Product Limited (TBPL) kilichopo Kibaha, Pwani.