Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bw. Godfrey Nyaisa akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 5, 2025 jijini Dar es Salaam.
………….
Msajili wa Kampuni amefuta Kampuni 11 kwa kukiuka masharti ya kifungu cha 400A (1) (e) cha Sheria ya Kampuni Sura 212 kwa kufanya shughuli za kibiashara nje ya madhumuni yaliyoainishwa katika Katiba za Kampuni hizo na miongozo ya Uendeshaji wa Kampuni wakati wa usajili.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 5, 2025, jijini Dar es Salaam Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Godfrey Nyaisa, amesema kifungu cha sheria kikikiukwa inamtaka Msajili, kuchukua hatua chini ya kifungu 400A (1) (e) ambacho ni kuijulisha kampuni kuhusu ukiukwaji na hatua anazokusudia kuzichukua kwa kampuni husika.
“Sheria inaendelea kueleza kuwa, endapo Kampuni itashindwa kutoa maelezo, au kutoa maelezo yasiyoridhisha, Msajili atafuta Kampuni husika kwenye Rejista ya Kampuni,”.
Hivyo Nyaisa amebainisha kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 400A (1) (e) Msajili alizijulisha Kampuni husika kuhusu kusudio la kuzifuta kupitia notisi zilizotolewa kati ya Januari 2 na 26 Mwaka huu.
Kwamba kwa kuwa Kampuni hizo hazikuwasilisha maelezo yoyote kama zilivyotakiwa chini ya kifungu 400A (2), Msajili amezifuta rasmi Kampuni hizo kuanzia Februari 27 Mwaka huu ambazo amezitaja kuwa ni LBL Mtwara Media Company Limited (Na. 181289972) na LBL Morogoro Media Company Limited (Na. 179770873).
Nyingine ni LBL Geita Advertising Media Limited (Na. 180439242), LBL Mbeya Media Limited (Na. 179978326), LBL Future Vision Advertising Agency Company Limited (Na. 181302259) na LBL Mbezi Advertising Media Company Limited (Na. 180582835).
Nyaisa ameongeza Kampuni nyingine kuwa ni LBL Ubungo Media Limited (Na. 180960333), LBL Mabibo Media Company Limited (Na. 181117346), LBL Mbagala Media Company Limited (Na. 181248874), LBL Gongo la Mboto Media Advertising Limited (Na. 181513438) na LBL Dar es Kigamboni Advertising Company Limited (Na. 180046992).
“Msajili anapenda umma ufahamu kwamba, hakuna Sheria wala Taasisi yenye Mamlaka ya kutoa vibali wala leseni za kufanya biashara za upatu za upatu hapa Nchini,” ameeleza Nyaisa.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Brela Nyaisa ameongeza kuwa, Msajili anaendelea na ufuatiliaji wa Kampuni nyingine zinazofanya shughuli za biashara nje ya Katiba zao na kinyume na Sheria na taratibu na ataendelea kuzichukulia hatua stahiki ikiwemo kuzifuta kwenye Rejista ya Kampuni.
Kwamba Msajili amekumbusha kuwa, biashara ya upatu ni kinyume na Sheria za Nchi, hivyo amewahimiza Wananchi kutoa taarifa mara Moja Kwa Mamlaka husika zikiwemo Taasisi za kiserikali na Jeshi la Polisi ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya Kampuni au watu wanaofanya au kujihusisha na biashara hiyo.