………………………..
Na Sixmund Begashe – Serengeti
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Maliasili Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba akiwa njiani kuelekea Hifadhi ya Taifa Serengeti amefanya ziara ya kushtukiza katika Lango la Nabi la Hifadhi ya Taifa Serengeti Kisha kukagua miundombinu pamoja na huduma zinazotolewa kwa wageni.
Akiwa katika ukaguzi kwenye eneo hilo, alifarijika kusikia kutoka kwa madereva wa magari ya watalii kuwa wanarizishwa sana na huduma wanazopatiwa kwenye mageti yote mawili (Serengetina Ngorongoro) yanayopatikana sehemu hiyo, huku akiwahakikishia madereva hao kuwa Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kufanya maboresho kwenye Hifadhi zote hapa nchini ili kuondoa changamoto zote kubwa na ndogo zilizobaki ikiwemo miundombinu ya barabara.
Aidha CP. Wakulyamba aliupongeza uongozi wa Hifadhi hizo kwa kazi nzuri ya usimamizi wa rasilimali zilizopo na kwa ubora wa huduma wanayoitoa hasa inayopelekea Uhifadhi salama wa Maliasili.
Kamishna Wakulyamba licha ya kuwapongeza, amewaagiza Viongozi hao kutatua changamoto iliyotolewa na baadhi ya madereva kwenye baadhi ya maeneo hifadhini ya kutokuwa na na alama za kuelekeza uelekeo.
Amewataka mara moja kuweka au kuongeza alama kwenye njia za Hifadhini ili kuondoa adha ya kutofika maeneo wanayotaka kwenda au kujikuta wamepotea na kuadhibiwa kwa kukiuka sheria za Hifadhi.
CP. Wakulyamba, akiwa kwenye ziara ya kikazi kwenye Hifadhi ya Taifa Serengeti, amepokelewa na Naibu Kamishna wa Uhifadhi, anayesimamia Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara, Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Massana Mwishawa, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Serengeti Stephano Msumi pamoja na Maafisa wengine wa TANAPA.