Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Awadh Ali Said akizungumza na Mawakala wa Vyama vya Siasa mara baada ya kuwasili katika Kituo cha Kujiandikisha Kupiga Kura Shehia ya Sokoni wakati alipofanya ziara Vituo mbalimbali na kutatua Changamoto zilizojitokeza Wilaya ya Magharibi B Unguja.



……………..
Na Rahma Khamis 4/3/2025
Jumla ya wapiga kura wapya 15,787 wameandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura Wilaya ya Magharibi A’ ambapo idadi hiyo imeongezeka ukilinganisha na makadirio yaliyoweka na kuvuka kiwango.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC Jaji George Joseph Kazi ameyasema hayo Skuli ya Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi ‘B’wakati akitembelea vituo vya uandikishaji wapiga kura ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kuvitembelea vituo hivyo.
Amesema kuwa walikadiria kuandikisha wapiga kura wapya 12,755 katika awamu yapili, hali hiyo imevuka malengo kinyume na walivyotarajia kwani inaonyesha kuwa wananchi wengi wamehamasika kujitokeza kuandikisha katika daftari hilo ukilinganisha na awamu zilizopita.
“Wananchi wengi wamehamasika kujiandikisha kwani awamu zilizopita hawakujitokeza kama mwaka huu”, alisema .
Ameeleza kuwa zoezi limekwenda vizuri kwa salama na Amani kwani na hakuna tatizo lolote hadi kukamilika kwake hapo jana Mach 3.
Akizungumzia kuhusu uandikishaji Wilaya ya Magharibi ‘B’ Jaji Kazi amesema zoezi limeanza vizuri hakuna dosari iliyojitokeza na wanatarajia kumaliza kama lilivyopangwa.
Jaji amefahamisha kuwa Tume imeweka waangalizi maalum katika vituo vya uandikishaji wapiga ili kuangalia hali ya uandikishaji inavyoendelea pamoja na utaratibu.
“Waangalizi hawa wapo kwa ajili ya kuangalia hali inavyokwenda tu, na sio kufanya kazi nyengine kama vile kusimamia na kutoa maelekezo”, alifafanua Jaji Kazi.
Nao Mawakala katika vituo hivyo wameiomba Tume ya Uchaguzi kutoa taarifa kwa masheha kuwafahamu watu wao ili kuepuka usumbufu.
Kwa upande wao wasimamizi wa Vituo hivyo wamesema kuwa vituo vimefunguliwa kwa wakati na zoezi limeanza vizuri hakuna tatizo lilijitokeza.
Katika ziara hiyo vituo mbalimbali vimetembelewa ikiwemo Skuli ya Urafiki, Skuli ya Kiembesamaki ,Shehia ya Melinne, Shehia ya Tomondo, Shehia ya Kwa Mchina na Shehia ya Mombasa.