Farida Mangube, Morogoro
WATU watatu wamefariki Dunia mkoani Morogoro kutokana na ajali ya magari mawili ya mizigo kugongana na kuteketea kwa moto.
Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Alex Mkama amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Machi 04, 2025 katika eneo la Nanenane barabara kuu ya Morogoro – Dar es Salaam, kata ya Tungi, Manispaa ya Morogoro.
Amesema magari mawili ya mizigo yamegongana uso kwa uso wakati yakiwa yanapishana kwenye tuta la kupunguza mwendokasi ambapo baada ya kugongana yameshika moto na kuteketea na kusababisha vifo vya madereva wote wawili na abiria mmoja.
Amesema kati ya magari hayo, mojawapo lilikuwa limebeba shehena ya mafuta yaliyotambuliwa kuwa ni diesel ambalo lina namba za usajili RL 6652 ya nchini Rwanda na imeteketea kwa moto na gari namba T.374 DLC Scania Continental mali ya Reliable Company.
Amesema Kikosi cha uokoaji na Zimamoto na vyombo vingine vya usalama vimejitahidi kudhibiti moto huo na kutoleta madhara zaidi.
Alisema uchunguzi eneo la tukio umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni dereva wa gari ambalo lilikuwa linatokea upande wa Morogoro kwenda Dar es Salaam ambalo lilikuwa tupu kushindwa kudhibiti mwendo na gari lake hivyo kuhamia upande wa mwenzake ambaye alikuwa akitokea Dar es Salaam kwenda Morogoro akiwa amebeba shehena ya Mafuta.
Amesema Miili yote mitatu imehifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti hospitali ya rufaa mkoani Morogoro.
Amesema jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linatoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kupunguza mwendo maeneo yanayomtaka kufanya hivyo ili kuzuia ajali zinazosababishwa na uzembe wa madereva