Na Prisca Libaga Arusha
04/3/2025 Wanawake, wajawazito na watoto 178 wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika zoezi la upimaji wa magonjwa hayo linalofanyika jijini Arusha katika maonesho ya kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Wanawake.
Upimaji huo wa siku nane unafanywa na wataalamu wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha katika viwanja vya TBA Kaloleni karibu na Mnara wa Mwenge mkabala na Makumbusho ya Taifa Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Arusha daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto na Mkuu wa Kitengo cha Utoaji wa Huduma Bora wa Taasisi hiyo Dkt. Naiz Majani alisema leo ni siku ya tatu tangu wameanza kufanya upimaji huo na wameona wanawake 88, wajawazito 42 na watoto 48.
Dkt. Naiz alisema katika upimaji huo wamewapima wanawake wajawazito kipimo cha Echokadiografia ya moyo wa mtoto aliyepo tumboni, kipimo hicho kinamsaidia mama kutambua afya ya moyo wa mtoto wake kabla hajajifungua kwani ni muhimu kwa wajawazito kufanya uchunguzi wa afya ya moyo wa mtoto awapo tumboni ili wataalamu wajue namna ya kutatua tatizo la mtoto kama anashida katika hatua za awali.
“Wanawake na watoto tuliowapima na kuwakuta na matatizo mbalimbali ya moyo walikuwa 29 kati ya hao watu wazima 26 na watoto watatu, sita kati yao watu wazima wakiwa wanne na watoto wawili tumewapa rufaa ya kuja kufanyiwa uchunguzi zaidi na kupata matibabu ya kibingwa katika taasisi yetu iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam”, alisema Dkt. Naiz.
“Kati ya wajawazito 42 tuliowafanyia kipimo cha Echokariografia ya moyo wa mtoto aliyepo tumboni watoto watatu tumewakuta na shida ya moyo na tumeandika barua maalumu ya rufaa kwenda katika hospitali watakazo jifungulia na tumechukuwa taarifa zao na tarehe watakazo jifungua, tutaendelea kuwafuatilia ili kujua maendeleo ya watoto hao ikiwa ni pamoja na kuanzishiwa matibabu mapema”.
“Tupo hapa kwa lengo la kupima watoto ambao wanadalili za magonjwa ya moyo au wazazi wanaotaka kufahamu afya za watoto wao, kikubwa zaidi taasisi yetu imekuja kufanya uzinduzi wa kampeni maalumu ya kugundua magonjwa ya moyo kwa watoto wakiwa tumboni,kampeni hii ni muhimu sana kwani kugundua mtoto ana maradhi gani akiwa tumboni kutasaidia kaanzishiwa matibabu sahihi na kwa haraka”, alisema Dkt. Naiz.
Dkt. Naiz alisema katika matibabu ya maradhi ya moyo wanayotoa JKCI wamebaini magonjwa mengi ya moyo kwa watoto kama yangegundulika mapema watoto hao wangetibiwa mapema na kupona.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo wakazi wa Arusha walifurahi kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa imewapa nafasi ya kupima na kutambua afya za mioyo yao.
Willian Mute mkazi wa Kaloleni alisema alikuwa na tatizo la moyo kwenda mbio baada ya kufanyiwa vipimo vya katika hospitali ya Mount Meru alikutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu na kuanzishiwa dawa ila baada ya kusikia kuna wataalamu wa moyo wako jijini Arusha akaona atumie nafasi hiyo kupima tena afya ya moyo wake.
“Nimepima kipimo cha kuangalia jinsi moyo wangu unavyofanya kazi nimekutwa uko sawa na sasa hivi nasubiri kufanyiwa kipimo cha mfumo wa umeme wa moyo. Nashukuru sana kwa huduma hii kwani nimeipata bila malipo yoyote yale”, alisema Mute.
“Nashukuru sana nimepima afya ya moyo wa mtoto wangu aliyepo tumboni namshukuru Mungu yuko salama, nawaomba kinamama wenzangu ambao ni wajawazito watumie nafasi hii kupima na kutambua afya za mioyo ya watoto wao ili kama watakutwa na shida ya moyo waanze matibabu mapema mara baada ya kuzaliwa”, alishukuru Mariam Juma mkazi wa Mianzini.