* Dkt. Biteko: Wanawake ni nguzo muhimu katika mapinduzi ya nishati safi
* Serikali kuimarisha sera na mikopo nafuu kwa biashara za nishati safi
* TANESCO yasisitiza umeme kuwa suluhisho la nishati safi ya kupikia
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amewataka wanawake nchini kuwa chachu ya mabadiliko kwa kuhamasisha na kutumia nishati safi ya kupikia, ikiwa ni hatua muhimu katika kulinda afya ya jamii na mazingira.
Akizungumza Machi 4, 2025, jijini Dar es Salaam kwenye Kongamano la Kuhamasisha Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa Umeme, Dkt. Biteko alisema wanawake wana nafasi kubwa katika kuleta mageuzi ya nishati safi nchini.
“Wanawake ni msingi wa familia na jamii, hivyo mchango wao katika kusukuma ajenda ya nishati safi ya kupikia ni wa muhimu sana. Hili ni suala ambalo Mheshimiwa Rais amelipa kipaumbele, nasi kama serikali tunahakikisha tunatoa mazingira bora ya kufanikisha mabadiliko haya,” alisema Dkt. Biteko.
Amesema ili kufanikisha malengo ya kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, serikali inaendelea kuboresha sera na sheria zinazohamasisha uwekezaji katika sekta hiyo.
Aidha, serikali itahakikisha wanawake wanapata fursa za mikopo nafuu kupitia mfuko wa Nishati Safi ya Kupikia ili waweze kushiriki kikamilifu katika biashara za nishati safi, hatua itakayochochea upatikanaji wa nishati hiyo kwa gharama nafuu zaidi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, amewahimiza wanawake kuwa mstari wa mbele katika kuelimisha jamii kuhusu faida za nishati safi ya kupikia na kusaidia kufanikisha mpango wa kitaifa wa kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mha. Gissima Nyamo-Hanga, amesema kuwa matumizi ya umeme kwa kupikia ni suluhisho endelevu kwa kuwa gharama zake zimekuwa nafuu na umeme umesambazwa katika maeneo mengi zaidi nchini.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, Mhe. Balozi Zuhura Bundala, aliongeza kuwa wanawake wanapaswa kutumia fursa hii kubadili mtazamo wa familia zao na jamii kuhusu nishati safi ya kupikia, kwani inasaidia kuboresha afya na kupunguza uharibifu wa mazingira.
Jukwaa hilo limeweka mkazo katika kuhakikisha wanawake wanakuwa wahamasishaji wa nishati safi ya kupikia, ikiwa ni hatua ya kuifanya Tanzania kuongoza katika mapinduzi ya nishati endelevu barani Afrika.