*Mradi wa Epanko Graphite Kuinufaisha Tanzania Kibiashara, Kiuchumi
*Kuchangia Zaidi ya Shilingi Trilioni 5 kwenye Pato la Taifa
*Tanzania kuwa Kiungo Muhimu Katika Sekta ya Nishati Safi Duniani
Tanzania imeandika historia mpya katika Sekta ya Madini baada ya Machi 3, 2025, Serikali kutoa Leseni Kubwa ya Uchimbaji (Special Mining Lisence- SML) wa Madini ya Kinywe (Graphite) kwa Kampuni ya EcoGraf Limited kupitia Mgodi wa Epanko Graphite, uliopo Kijiji cha Epanko Wilaya ya Mahenge, Mkoani Morogoro.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa Serikali wa kuboresha Sekta ya Madini hapa nchini sambamba na kuongeza thamani kwa maliasili zake ikiwemo za madini ambako Mradi huo unatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika uchumi, viwanda, ajira, na nafasi ya Tanzania katika soko la kimataifa la nishati safi.
Katika taarifa yake kwa umma, Mkurugenzi Mtendaji wa EcoGraf, Andrew Spinks amesema kuwa Serikali ya Tanzania ilifanya tathmini ya kina ya maendeleo ya Mradi wa Epanko na kwamba Kampuni hiyo inatoa shukraniza dhati kwa Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, kwa msaada wao na kwa kuidhinisha utolewaji wa leseni hiyo.
*Mapato Makubwa kwa Serikali na Uwekezaji Endelevu
Serikali ya Tanzania itanufaika na kodi na tozo mbalimbali zitakazotokana na shughuli za mgodi wa Epanko. Mapato hayo yanaweza kuelekezwa katika miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa shule, hospitali, barabara, na miradi mingine ya kijamii.
Licha ya dola milioni 850 sawa na shilingi trilioni 2.1 zinazotarajiwa kulipwa na kampuni hiyo kama kodi, gawio, ada, mrabaha na ununuzi wa huduma na bidhaa tofauti katika kipindi cha kuendesha shughuli zake, inakadiriwa itachangia zaidi ya dola bilioni 2.5 sawa na shilingi trilioni 5.6 kwenye pato la Taifa (GDP).
*Mapinduzi ya Sekta ya Viwanda na Ongezeko la Thamani kwa Madini Kinywe (Graphite)
“Hatua hii inafanya Mradi wa Epanko kuwa mradi mkubwa zaidi ya madini kinywe barani Afrika ambao upo tayari kuendelezwa. Akiba ya madini kinywe ya Epanko (Ore Reserve) inakadiriwa kuwa tani 290.8 Mt, ikitoa uhakika mkubwa katika uendelezaji wa madini, ubora wa madini yatakayosafishwa, mambo ambayo ni muhimu katika kuamua bei sokoni” imesema taarifa hiyo.
Epanko Graphite itahakikisha kwamba uchakataji wake unafanyika hapa nchini kabla ya kusafirishwa nje huku Tanzania ikijitengenezea nafasi ya kuwa kitovu cha uzalishaji wa madini hayo yenye thamani ya juu, ambayo ni malighafi muhimu kwa utengenezaji wa betri za magari ya umeme na mifumo ya kuhifadhi nishati mbadala.
“Utolewaji wa Leseni Kubwa ya Uchimbaji (SML) ni hatua muhimu katika maendeleo ya Epanko na sharti kuu kwa mchakato wa ufadhili, ambao utasaidia hatua ya kwanza ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha kuchenjua grafiti chenye uwezo wa kuzalisha tani 73,000 kwa mwaka.” Imeongeza taarifa hiyo.
*Tanzania kuwa Kiungo Muhimu Katika Sekta ya Nishati Safi Duniani
Dunia inashuhudia mageuzi makubwa ya kuachana na nishati ya mafuta na kuelekea kwenye nishati safi. Magari ya umeme na mifumo ya kuhifadhi nishati ya jua na upepo vinahitaji betri bora zenye uwezo mkubwa wa kuhifadhi chaji kwa muda mrefu. Madini ya Kinywe (Graphite) ni moja ya malighafi muhimu zaidi katika utengenezaji wa betri hizo, na mradi wa Epanko utaiweka Tanzania katika nafasi ya kimkakati kama mtoa huduma wa malighafi hii kwa masoko ya makubwa ya Ulaya, Asia, na Amerika Kaskazini.
Kwa kuzingatia kuwa Madini ya Kinywe ya Tanzania ni ya kiwango cha juu, nchi inaweza kuwa moja ya wazalishaji wakubwa duniani, hivyo kuongeza nguvu ya Tanzania katika soko la kimataifa la betri za umeme. Ndani ya kipindi kifupi inaweza kuongeza nafasi ya Tanzania katika diplomasia ya kiuchumi, kwani nchi zilizoendelea zinauhitaji mkubwa wa malighafi hiyo.
*Ajira na Uboreshaji wa Maisha ya Watanzania
Moja ya manufaa makubwa ya mradi wa Epanko ni kuongeza fursa za ajira kwa maelfu ya Watanzania. Mradi huo hautahusisha tu uchimbaji wa madini, bali pia usindikaji wake, usafirishaji, na huduma za kusaidia shughuli za mgodi kama vile chakula, usafiri, na ulinzi. Hii inamaanisha kuwa wataalamu wa migodi, wahandisi, madereva, mafundi, wachimbaji, na wafanyabiashara wa huduma watafaidika moja kwa moja na mradi huu.
Kwa kuzingatia kuwa mgodi huu unapanua eneo lake kutoka 9.6 km² hadi 18.9 km², inamaanisha kuwa kuna fursa kubwa zaidi za ajira kwa Watanzania wengi, hasa kutoka jamii zinazozunguka mgodi. Zaidi ya hayo, kampuni ya EcoGraf inatarajia kutoa mafunzo kwa vijana wa Kitanzania ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za mgodi kwa kutumia teknolojia za kisasa.
Kwa upande mwingine, sekta ya biashara za ndani pia itanufaika, kwani kutakuwa na ongezeko la mahitaji ya bidhaa na huduma kama vile malazi, chakula, vifaa vya ujenzi, na vifaa vya uchimbaji. Hii itaimarisha uchumi wa ndani na kuchochea maendeleo katika sekta mbalimbali.
Mradi wa Epanko Graphite siyo tu fursa ya kiuchumi kwa Tanzania, bali ni hatua muhimu kuelekea mapinduzi ya sekta ya madini na viwanda. Kupitia ajira, maendeleo ya viwanda, uuzaji wa bidhaa zenye thamani ya juu, na nafasi ya kimataifa kwenye sekta ya nishati safi, Tanzania inajiimarisha kama mshindani mkubwa katika soko la kimataifa la graphite.