Na. Mwandishi wetu Jeshi la Polisi.
Jeshi la Polisi la Mkoa wa Arusha kupitia mtandao wa Polisi Wanawake limetoa msaada wa vitu mbalimbali kwa Wanafunzi wenye ulemavu wanaosoma katika kituo cha Mafunzo kwa Watu wenye ulemavu kilichopo wilaya ya Arumeru mkoani humo.
Mwenyekiti wa mtandao wa Polisi wanawake Mkoa wa Arusha (TPF NET) Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Debor Lukololo amesema kuwa Jeshi hilo kupitia mtandao huo limetoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwa mwendelezo wa shamrashamra kuelekea siku ya Wanawake Duniani itakayofanyika kitaifa mkoani humo.
ACP Lukololo amebainisha kuwa kuelekea siku ya Wanawake duniani wameona ni vyema kutoa sadaka kwa wanafunzi hao walemavu ambao wanauhitaji katika jamii huku akitaja baadhi ya vitu hivyo kuwa ni magodoro, sukari, mchele, taulo za kike na vitu vingine vingi ambavyo ni vya muhimu kwao.
Aidha ametoa wito kwa taasisi nyingine za kiserikali na zisizo za Kiserikali kuwa na utaratibu wa kuwakumbuka watu wenye uhitaji katika jamii kwani kwa kufanya hivyo kutawafariji watu hao lakini pia watapata baraka kutoka kwa Mungu.
Kwa upande wake Mkuu wa Kituo hicho Mwalimu Emmanuel Ayo amesema Kituo hicho kilianzishwa mwaka 1988 lengo likiwa ni kuwasaidia watu wenye ulemavu ili waweze kupata ujuzi ambao utawasaidia kuwaepusha kuwa wategemezi kwa familia zao ambapo mpaka sasa kina wanafunzi 214.
Nao wanafunzi baada ya kupokea msaada huo wametoa shukrani za dhati kwa mtandao huo kwa msaada waliotoa na kuwaombea kwa Mungu.