Mwamvua Mwinyi, Chalinze
Februari 4, 2025
Ofisa Ardhi Halmashauri ya Chalinze mkoani Pwani, Baltazar Mitti, ameeleza kuwa kero nyingi za migogoro ya ardhi zinatokana na wananchi kutokuwa na uelewa wa kisheria, hali inayosababisha kutapeliwa au kudhulumiwa.
Akitoa elimu kuhusu Sheria ya Ardhi kwa wananchi wa vijiji vya Milo, Buyuni, na Vigwaza, katika ziara ya maofisa kutoka Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, Halmashauri ya Chalinze pamoja na Wizara ya Sheria na Katiba, alisisitiza kufuata taratibu sahihi za ununuzi na umiliki wa ardhi
Alisisitiza umuhimu wa kufuata taratibu za kisheria wakati wa mauziano ya ardhi, ikiwa ni pamoja na kutumia mikataba rasmi na kushirikisha viongozi wa kijiji ili kupunguza migogoro isiyo ya lazima.
Mitti alieleza ,wapo baadhi ya watu ambao wanatapeliana, hata ndugu kwa ndugu, katika masuala ya mirathi ,hivyo, alishauri endapo kutatokea kifo, ni vyema kufuata taratibu za kupata mirathi.
Alitoa ushauri kwa jamii kabla ya kukimbilia mahakamani mara moja wanapokutana na migogoro ya ardhi watumie njia za mazungumzo ya kisheria na upatanisho ili kutatua migogoro kwa amani.
Vilevile, alikumbusha wananchi kufuata sheria, kwani misingi ya kisheria inaonyesha kuwa wengi wanatenda jinai, hali inayochochea migogoro ya ardhi.
Mitti aliwasihi wananchi waache kuvamia maeneo yenye umiliki halali ili kuepuka migogoro.
Aliongeza kuwa migogoro mingine iliyoripotiwa ni ile ya wakulima na wafugaji, ambapo aliwataka kuheshimu mipaka ya maeneo, hasa kwa wale walioko katika maeneo yenye mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Mkazi wa kijiji cha Milo, Thabit Rashid, na Adam Muhammed walieleza ukosefu wa elimu kuhusu sheria mbalimbali, unachangia kwa kiasi kikubwa watu wengi kukosa haki zao za msingi.
Walishukuru kwa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, wakisema kuwa imekuja wakati muafaka.
Malki Paulo alieleza changamoto ya ukosefu wa maji, miundombinu ya barabara, na tatizo la wafugaji holela kuchunga mifugo kwenye mashamba ya wakulima, hali inayosababisha wakulima kupoteza mazao yao.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa Chalinze, Atuganile Chisunga, alifafanua lengo la kampeni hiyo ni kutoa elimu na msaada wa kisheria kwa wananchi katika masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kusaidia wale wenye kesi mahakamani lakini hawana uwezo wa mawakili, kwa kuwapatia ushauri wa kisheria.