* Dkt. Biteko: Afrika inachukua hatua madhubuti kuhamasisha nishati safi
* Mjadala wa Nishati Safi waangazia pia usafiri na matumizi ya majumbani
* Serikali ya Tanzania yaendelea kuboresha sera na uwekezaji katika gesi asilia
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amesema kuwa Afrika imeendelea kuwa kinara katika juhudi za kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuimarisha sera na sheria zinazohamasisha matumizi ya nishati safi.
Akizungumza Machi 4, 2025, wakati wa kufungua Mkutano wa Awali wa Kongamano la Mafuta na Gesi la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAPCE’25), Dkt. Biteko alisisitiza umuhimu wa mkutano huo katika kujadili mikakati ya kuimarisha matumizi ya nishati safi, hususan katika sekta ya usafiri na matumizi ya majumbani.
“Lazima tutambue kuwa Afrika haichangii kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira, lakini tumejikita kikamilifu katika kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa kuhakikisha tunahama kutoka nishati chafu kwenda nishati safi,” alisema Dkt. Biteko.
Akitolea mfano sekta ya upishi, alisema kuwa Afrika bado inakabiliwa na changamoto kubwa kwani zaidi ya asilimia 80 ya kaya nchini Tanzania zinatumia kuni na mkaa, hali inayosababisha uharibifu wa misitu. Ili kukabiliana na tatizo hilo, Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameanzisha Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034) unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.
Pamoja na hilo, Dkt. Biteko alisisitiza kuwa Afrika ni bara lenye changamoto kubwa ya upatikanaji wa nishati, ambapo asilimia 75 ya watu wasiokuwa na nishati duniani wanapatikana barani humo. Hata hivyo, kupitia mikakati kama ilivyojadiliwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati uliofanyika Tanzania Januari 2025, jitihada zinaendelea kuwekwa kuhakikisha mamilioni ya Waafrika wanapata umeme ifikapo 2030.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, alisema mkutano wa EAPCE’25 ni jukwaa muhimu kwa wadau wa sekta ya mafuta na gesi, kwani unatoa fursa ya kujadili hatua zilizopigwa na fursa za uwekezaji.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, aliongeza kuwa mkutano huo pia umeangazia maendeleo katika sekta ya gesi asilia, hususan matumizi ya Gesi Asilia Iliyoshindiliwa (CNG) kwa usafiri wa umma, ikiwa ni moja ya hatua za kuhamia nishati safi.
Mkutano wa EAPCE’25 utaendelea kwa siku tatu, ukihusisha wataalamu, watafiti, na wawekezaji wa sekta ya mafuta na gesi, huku lengo kuu likiwa ni kuweka mikakati ya Afrika Mashariki kuelekea kwenye uchumi wa kijani na maendeleo endelevu.