Mratibu wa Programu ya Lipa kwa Matokeo (PforR) kutoka Wizara ya Maji, Mhandisi Mashaka Sita, pamoja na timu ya Benki ya Dunia, wamekagua hali ya huduma ya maji katika Wilaya ya Chamwino. Ukaguzi huo ulifanyika katika Chombo cha Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii Mvumi Mission, ambacho kimepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma na kupanua mtandao wa maji ili kuwafikia wananchi wengi zaidi. Hivi sasa, huduma ya maji inapatikana kwa saa 12 kwa siku.
Mhandisi Sita alisisitiza kuwa moja ya viwango vya kupima ubora wa huduma ya maji ni kuhakikisha kuwa kujaza ndoo moja ya maji hakuzidi dakika tano. “Kujaza maji ndoo moja inapaswa kuchukua chini ya dakika tano, na isizidi,” alieleza, akibainisha kuwa kigezo hiki kinatumika kupima ubora wa huduma katika jamii.
Diwani wa Mvumi, Mhe. Keneth Chiute, aliipongeza programu hiyo kwa kupunguza changamoto za upatikanaji wa maji, huku akiomba juhudi zaidi ili kuhakikisha wananchi wote katika maeneo ya pembezoni pia wananufaika na mradi huo.
Naye Diwani wa Viti Maalum, Mhe. Shukran Chelea, alibainisha kuwa programu ya PforR imeleta utulivu ndani ya familia, kwani awali maji yalihitajika kutafutwa nyakati za usiku bila uhakika wa kupatikana. “Sasa hali ni bora zaidi, mahitaji ya familia yanakidhiwa kwa wakati, na ndoa nyingi zimeimarika kutokana na upatikanaji wa maji wa uhakika,” alisema.
Vyanzo vya maji katika Wilaya ya Chamwino vinapatikana chini ya ardhi, hivyo utunzaji wa mazingira umetajwa kuwa muhimu kwa ajili ya kudumisha huduma endelevu ya maji kwa jamii.
Ukaguzi wa utekelezaji wa programu ya PforR umeongozwa na Bi. Toyoko Kodama kutoka Benki ya Dunia, Marekani. Tanzania imefanya vizuri katika programu hii na imekuwa mfano wa kuigwa na mataifa mengine duniani katika utoaji wa huduma bora za maji kwa wananchi.