Na: Happiness Sam – Manyara, Tanzania
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania TANAPA limeendelea kuhamasisha watanzania hususani wanawake ambalo ni jeshi kubwa, kutembelea vivutio vya utalii vilivyomo ndani ya Hifadhi za Taifa kwani utalii unafaida nyingi zikiwemo afya, elimu, kujenga mshikamano na kuchangia katika uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa wiki ya kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani katika Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara Machi 1, 2025, Naibu Kamishna wa Uhifadhi Steria Ndaga ambaye ni Mkuu wa Kanda ya Kaskazini, alisema kuwa TANAPA imejipanga kuhakikisha watanzania, hususani wanawake wanapata fursa ya kutembelea vivutio vya asili vilivyopo Nchini.
“TANAPA inatambua mchango wa wanawake katika uhifadhi wa maliasili na maendeleo ya utalii katika Taifa letu, tunawahamasisha wanawake kutumia fursa hii ya sikukuu ya wanawake Duniani kujifunza zaidi, kupata utulivu wa akili sambamba na kusaidia kuongeza pato la nchi,” alisema Kamishna Ndaga.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt.Yustina Kiwango, ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara alibainisha kuwa gharama za kiingilio kwa watanzania ni Sh 11,800, huku ada ya gari ikiwa kati ya Sh 23,600 hadi 41,300 kulingana na uzito wa gari, hatua inayolenga kuhakikisha utalii unakuwa nafuu na kufikika kwa kila Mtanzania.
Katika maadhimisho hayo, wanawake walishiriki katika shughuli mbalimbali za utalii ikiwemo matembezi juu ya kamba (canopy walk), safari za kupiga kasia ziwani na kuona makundi makubwa ya wanyama, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa TANAPA kuhamasisha utalii wa ndani hususani kwa wanawake.
Maadhimisho hayo ambayo yalifana kwa sherehe zilizowakutanisha watumishi wanawake zaidi ya 150 kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania TANAPA wakisherehekea mchango wao katika uhifadhi na maendeleo ya Taifa kupitia utalii wa ndani ,yanatarajiwa kuhitimishwa mnamo Machi 08, 2025.