Benki ya NMB Kanda ya Ziwa imetoa vifaa tiba katika hospitali ya Kanda Chato pamoja na kuchangia vifaa katika sekta ya elimu kwa Shule nne za Chato Mkoani Geita na mbili za Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 37.
Vifaa hivyo vimetolewa na kukabidhiwa na Meneja wa NMB kanda ya Ziwa Faraja Ng’ingo kwa awamu mbili tofauti ambapo awamu ya Kwanza imetolewa Wilayani Chato katika Shule ya Msingi Mkuyuni.
Vifaa vilivyotolewa katika sekta ya elimu ni pamoja na madawati 150, Viti na Meza 50, Kompyuta tatu vilivyotolewa Wilayani Chato pamoja na viti mwendo na mabati 200 kwa shule za msingi Kaigara na Biija za Wilayani Muleba.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo Ng’ingo amesema kama wadau wa maendeleo wameona warudishe kwa jamii sehemu ya faida waliyo ipata.
Amesema Benki hiyo imetoa Madawati 150 kwa shule za Itale, Mkuyuni na Rumasi huku shule ya Rubambagwe ikikabidhiwa viti na meza 50 na Kompyuta tatu kwa shule ya Rumasi.
Vifaa vingine ni vitanda 10 pamoja na magodoro yake, Viti mwendo 10 kwa ajili ya wagonjwa pamoja na mashine 10 za kupimia shinikizo la damu vilivyotolewa katika Hospitali ya Kanda Chato.
“Kwa miaka kadhaa sasa tumekua tukishirikiana na jamii kutatua baadhi ya changamoto katika sekta ya elimu, afya na pale inapotokea majanga kama mafuriko na moto tumekua tukirudisha kwa jamii na huwa tunatoa sehemu ya faida kuchangia kama sehemu ya uwajibikaji wetu kwa jamii inayotuzunguka,”amesema
Amesema Benki hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo huku ikirudisha sehemu ya faida yake kwa wananchi.
“Tunaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kusaidia upatikanaji wa elimu bora na kuboresha mazingira ya kazi kwa njia hiyo tunawafikia wananchi na wateja wetu kwa wingi”alisema Ng’ingo
Aidha viti mwendo vinne vilivyotolewa kwa shule jumuishi ya Kaigara,vitapunguza changamoto ya wanafunzi wenye ulemavu kukosa vifaa saidizi shuleni hapo
Mkuu wa Wilaya ya Muleba Abel Nyamahanga akipokea msaada huo amekemea vitendo vya ubaguzi kwa watoto wenye changamoto za maumbile na kuomba wadau zaidi wajitokeze kutoa mahitaji yao
“Wazazi tusifiche watoto wenye changamoto za viungo,hii ni shule inayotoa elimu Jumuishi watoto wanaponyanyaswa na kubaguliwa watadhani huo ndio utaratibu wa maisha wasinyanyaswe kwa namna yoyote”Alisema Nyamahanga
Kwa upande wake Katibu tawala wa Wilaya ya Chato Thomas Dime aliyemwakilisha Mkuu wa wilaya hiyo amesema msaada uliotolewa utapunguza changamoto ya madawati na kuishukuru NMB kwa kuwa mdau muhimu wa maendeleo ambae amekua akiisaidia Wilaya hiyo mara kwa mara.
“Pamoja na msaada ambao tumepata lakini tuna changamoto ya madawati zaidi ya 26,000 tunaendelea kutatua changamoto hii kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri”amesema Dime
Halmashauri kupitia mapato ya ndani tafuteni ufumbuzi wa tatizo hili mkishirikiana na kamati za shule ni wajibu wa wazazi kuchangia madawati,” amesema Dime
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mkuyuni Verena Nicolous amesema shule hiyo yenye wanafunzi 1,683 inaupungufu wa madawati 164 na kusema msaada waliopewa utakua chachu ya kunyanyua elimu kwenye shule hiyo.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Mkuyuni wamesema kukosekana kwa madawati husababisha baadhi kukaa chini na kwamba msaada uliotolewa na NMB utawasaidia kusoma kwenye mazingira rafiki.
Salum Ramadhan mwanafunzi wa darasa la saba amesema kutokana na vumbi wanafunzi wanachafuka na kuchafua madaftari na kuomba wadau wengine kusaidia ili waondokane na uhitaji wa madawati.
Kaimu Mkurugenzi wa hospitali ya rufaa ya kanda Chato Dk Osward Lyapa akizungumzia msaada wa vifaa tiba vilivyotolewa ikiwemo mashine ya kupimia shinikizo la damu,vitanda na viti mwendo itasaidia kuhudumia wagonjwa hususan kliniki za moyo zinazofanyika kwenye hospitali hiyo.
“Hivi karibuni tumekabidhiwa fedha z akukamilisha jengo letu la wodi na tutakuw ana uwezo w akulaza wagonjwa zaidi ya 200 kwa wakati mmoja kwa msaada huu hakutakua na wagonjwa wanaolala chini au wawili kwenye kitanda kimoja tunawashukuru sana kwa msaada huu,”amesema Lyapa
Afisa elimu wa Kata ya Muleba, Garib Issa akizungumzia misaada inayotolewa na NMB amesema Benki hiyo imekuwa ikisaidia mara kwa mara na tayari ilishatoa tena vitanda na magodoro katika shule hiyo ya Kaigara ambayo ndiyo pekee yenye kitengo cha elimu Jumuishi katika Wilaya ya Muleba.