Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini aliyepo kushoto akiwa amefuatana na Mkuu wa mkoa wa.Arusha ,Paul Makonda wakati akiwasili katika banda la wizara ya katiba na Sheria katika viwanja vya TBA mkoani Arusha .

Mkuu wa mkoa wa Arusha ,Paul Makonda akitoa maelezo kwa Naibu Waziri alipotembelea mabanda mbalimbali mkoani Arusha.


Wananchi mbalimbali mkoani Arusha wakiwa katika banda la wizara ya katiba na Sheria kwa ajili ya kupata msaada wa kisheria mkoani Arusha .
………….
Happy Lazaro, Arusha .
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini, amewataka wananchi kutoa maelezo sahihi kwa watoa huduma za msaada wa kisheria ili kufanikisha kutatua changamoto zinazowakumba, na kuhakikisha kuwa migogoro ya ardhi, mirathi, ndoa na masuala mengine ya kisheria yanapata ufumbuzi kwa wakati.
Sagini ameyasema hayo leo mkoani Arusha wakati alipotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na mabanda mengine kuelekea wiki ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ambayo itafanyika Machi 8 mwaka huu mkoani Arusha.
Aidha maadhimisho hayo ambayo yanatangulizwa na maonyesho kutoka kwa taasisi na mashirika mbalimbali, amewataka wananchi kutumia fursa hiyo kufika kwa wingi katika mabanda hayo kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za kisheria sambamba na kutatuliwa kero za zinazowakabili kwa wakati.
Aidha Sagini amekazia umuhimu wa kampeni ya Mama Samia Legal Aid inayolenga kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wenye changamoto za kisheria.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda ameagiza watoa huduma za msaada wa kisheria kwenye kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia, kuhakikisha kuwa wananchi wote waliofika kupata msaada wa kisheria wanasikilizwa na kutatuliwa changamoto zao kikamilifu.
Makonda amesema kuwa ,lengo la wananchi kufika kwenye mabanda hayo ni ili kupata haki zao za msingi kwa wakati na kutatuliwa kero zao kupitia kampeni ya Samia Legal Aid inayotolewa viwanja vya TBA.
Makonda amesema wananchi wanaofika katika banda hilo wanatakiwa kusikilizwa na kuhudumiwa ili waweze kutoa malalamiko yao ikiwemo kuangalia kwa makini changamoto zao hususani katika idara ya kazi, sheria, haki za watoto na mengineyo.
Aidha Makonda ametumia fursa hiyo pia kuwasihi wananchi wa mkoa wa Arusha kujitokeza kwa wingi kupatiwa msaada huo wa kisheria ili migogoro yao iweze kutatuliwa kupitia uwezeshaji uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan uliotokana na wazo lake hili la kuwa na kampeni ya kitaifa ili kuwafikia wananchi wanyonge na wale wanaokosa haki zao kulingana na sheria.
Nao baadhi ya wananchi waliofika kupata huduma kwenye banda hilo wamesema kuwa, wanashukuru serikali kwa kuwasogezea huduma karibu ili waweze kutatuliwa changamoto zao na kuweza kupata elimu zaidi kuhusu maswala ya kisheria ambayo yamekuwa ni changamoto kwa wengi wao kutokana na kutozijua sheria mbalimbali .
“Kwa kweli tunashukuru sana kwa jambo hili kwani limetupa fursa kubwa sisi kuweza kujifunza na hata kutatuliwa changamoto zetu ambazo zilikuwa zimedumu kwa muda mrefu na kuweza kupata huduma hiyo bure pia tunamshukuru sana Rais Samia kwa kua nzisha hii kampeni ambayo inalenga kutatua changamoto mbalimbali za mambo ya kisheria.”amesema.