Uganda
Naibu Katibu Mkuu wa chama tawala cha National Resistance Movement (NRM), nchini Uganda Mheshimiwa Namayanja Rose Nsereko, amewahimiza wakazi wa Nakaseke kujikita katika ufugaji wa kuku kama njia ya kuboresha maisha yao na kuchangia maendeleo ya taifa.
Namayanja alitoa wito huo jana alipokuwa akizungumza na wakulima wa Billionaires Club, kundi linaloendeshwa chini ya Kanisa la Waadventista wa Sabato (SDA). Akiwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Kande Poultry Farm iliyoko Semuto Town Council, Ssebagaala Zone katika Wilaya ya Nakaseke, Namayanja alishiriki safari yake ya kufanikisha ufugaji wa kuku zaidi ya 110,000 katika eneo lisilozidi ekari moja, akisema mafanikio yake yametokana na mbinu bora zinazozingatia rasilimali alizonazo.
“Katika eneo lisilozidi ekari moja, ninafuga zaidi ya kuku 110,000. Watu wanaweza kujiuliza inawezekanaje, lakini jibu ni rahisi sana. Natumia mfumo wa mabanda ya vyuma (cage system). Kwa kutumia mfumo huu, nimeokoa kiasi kikubwa cha chakula cha kuku na pia nimepunguza kwa kiwango kikubwa maambukizi ya magonjwa,” alisema Namayanja.