Dar es Salaam, Februari 28, 2025
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi, amesisitiza umuhimu wa teknolojia na utafiti wa kina katika kuongeza ufanisi wa uchunguzi na matibabu ya magonjwa adimu.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Magonjwa Adimu yaliyofanyika MNH, Prof. Janabi alisema kuwa matumizi ya akili bandia (AI) na nyenzo za kisasa za uchunguzi yanaweza kusaidia madaktari kupata utambuzi sahihi na kwa haraka.
“Kuimarisha ujuzi wa wataalamu wa afya kwa kutumia teknolojia mpya kutasaidia kuboresha matibabu na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora,” alisema Prof. Janabi.
Aliongeza kuwa ni muhimu kuendelea kuchapisha tafiti na nyenzo za elimu kuhusu magonjwa adimu ili kuhamasisha jamii na kutoa maarifa kwa madaktari, watoa huduma za afya, na familia za wagonjwa.
Daktari wa Watoto na Endocrinologist, Dkt. Kandi Muze, alieleza kuwa changamoto kubwa zinazowakabili wagonjwa wa magonjwa adimu ni upungufu wa rasilimali za matibabu na uelewa mdogo wa jamii.
“Msaada wa jamii na elimu sahihi vitasaidia wagonjwa na familia zao kupata mazingira bora ya matibabu na msaada wa kihisia,” alisema Dkt. Muze.
Katika maadhimisho hayo, Bw. Khamis Kaundu, ambaye binti yake Yusra ameishi na ugonjwa wa Gaucher tangu mwaka 2016, aliwashukuru madaktari wa Muhimbili kwa jitihada zao katika matibabu.
Kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya watu milioni 300 duniani kote wanakabiliwa na magonjwa adimu, huku asilimia 95 ya magonjwa hayo yakiwa hayana matibabu yaliyoidhinishwa. Wataalamu wanasisitiza kuwa uwekezaji katika utafiti na teknolojia utasaidia kuboresha hali ya wagonjwa na kupanua chaguzi za matibabu.