Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) imeeleza dhamira yake ya kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kutangaza utalii nchini kupitia mpango wa Royal Tour.
Akizungumza wakati wa ziara ya Maafisa Ushirika katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire tarehe 28 Februari 2025, Kaimu Naibu Mrajis wa Uhamasishaji, Consolata Kiluma, alisema kuwa ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Tume kuhakikisha Maafisa Ushirika wanaimarika katika utendaji kazi baada ya mafunzo ya usimamizi wa vyama vya ushirika kwa maafisa wa Kanda ya Kaskazini.
“Baada ya mafunzo haya, Tume iliona umuhimu wa kuwawezesha maafisa kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Tarangire ili kujionea vivutio vya utalii vinavyopatikana nchini. Hii siyo tu njia ya kuhamasisha utalii wa ndani, bali pia kusaidia kuboresha afya ya akili ya watumishi wetu, jambo linaloongeza ufanisi wanaporejea kwenye vituo vyao vya kazi,” alisema Kiluma.
Aliongeza kuwa TCDC itaendelea kuandaa ziara kama hizi katika hifadhi nyingine nchini ili Maafisa Ushirika waendelee kufahamu zaidi kuhusu rasilimali za taifa na kushiriki kikamilifu katika kuvitangaza vivutio vya utalii.
Kwa upande wake, Afisa Ushirika wa Mkoa wa Arusha, Neema Neman, aliishukuru Tume kwa kuona umuhimu wa ziara hiyo, akibainisha kuwa imewasaidia kupumzika, kujifunza, na kupata ari mpya ya kutekeleza majukumu yao ya usimamizi wa vyama vya ushirika.
Naye Mhifadhi wa Kitengo cha Utalii katika Hifadhi ya Taifa Tarangire, David Benedict, alieleza kufurahishwa na ziara hiyo na kupongeza hatua ya TCDC kuhamasisha watumishi wake kutembelea hifadhi hiyo.
“Kupumzisha akili ni jambo muhimu baada ya kazi. Tunakaribisha wageni wengine kutoka Tume ili waone na kufurahia uzuri wa vivutio vyetu vya asili,” alisema Benedict.