Na WAF – Moshi, Kilimanjaro
Serikali kupitia Wizara ya Afya imewekeza Shilingi Bilioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kituo cha tiba mionzi pamoja na ununuzi wa vifaa tiba lililopo katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Kaskazini (KCMC) ili kuboresha huduma hizo za afya na kuwafikia wananchi wengi wa ukanda huo.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Machi 1, 2025 alipofanya ziara katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Kaskazini (KCMC) ili kuona maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo linalotoa huduma za Saratani kwa njia ya tiba mionzi ambapo kwa ujumla ameridhishwa na ujenzi huo.
“Sekta ya Afya sisi sio washindani, bali tunashirikiana pamoja ili kuhakikisha tunatoa hudumu za afya zilizo bora kwa wananchi na kuwafikia wananchi wote,” amesema Waziri Mhagama.
Amesema, Kituo hicho cha tiba mionzi kitakua ni kati ya vituo vichache ambavyo vinatoa huduma za matibabu ya ugonjwa wa saratani kwa njia ya mionzi kutoka kwa wataalam wenye ubobezi na umahiri wa hali ya juu wa hapa nchini kwetu ambao wamesomeshwa kupitia ufadhili wa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Waziri Mhagama ameendelea kusisitiza juu ya umuhimu wa kuzingatia mtindo bora wa maisha kwa kuepuka matumizi mengi ya mafuta, sukari na chumvi ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kwa kuwa magonjwa hayo yamekuwa yakiongezeka.
“Tumekubaliana kama Serikali tutaendelea na kampeni ya hali ya juu kwa kutoa elimu juu ya magonjwa yasioyoambukiza ambayo yanatumia muda mrefu kwenye matibabu, fedha nyingi katika kuyatibu lakini pia yanahitaji uwekezaji mkubwa ambao utawezesha huduma hizi kutolewa inavyotakiwa,” amesema Waziri Mhagama.
Katika hatua nyingine, Waziri Mhagama amewataka wananchi wote kuendelea kuelimishana juu ya magonjwa ya milipuko kwa kuchukua tahadhari kwa kuwa magonjwa hayo yamekuwa yakijitokeza nchi za wenzetu.
Waziri Mhagama amesema ameridhishwa na ujenzi wa kituo hicho cha tiba mionzi ambacho kinatarajiwa kuanza kutoa huduma hizo mwezi Aprili mwaka huu (2025).