Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
Machi 1, 2025
Wananchi wa kata ya Miono na Mandela, Jimbo la Chalinze, mkoani Pwani wamebainisha kwamba, ukosefu wa elimu kuhusu sheria mbalimbali unachangia kwa kiasi kikubwa watu kukosa haki zao za msingi.
Wakazi wa Mandela wakizungumza wakati wa ziara ya maofisa kutoka Msaada wa Kisheria ya Mama Samia halmashauri ya Chalinze pamoja na Wizara ya Sheria na Katiba, Jafari Hassan na Hemed Abdallah Mbonde walieleza ,kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia imekuja wakati muafaka.
Jafari aliomba, serikali kupitia wizara ya katiba na sheria ama halmashauri iangalie uwezekano wa kuendeleza kampeni kama hiyo japo mara moja kwa mwaka.
Hemed Abdallah alieleza , wengi walikosa haki zao ,kwakuwa walikuwa hawana elimu ya umuhimu wa wosia, ardhi, na sheria ya ndoa lakini sasa wamepata fursa ya msaada wa kisheria.
“Msaada wa kisheria wa Mama Samia umekuwa mkombozi kwetu, Sasa tunafahamu sheria ambazo tulikuwa hatuzijui,” alisema Mohammed.
Asia Festus, Wakili na Mratibu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, akiwa Miono, alisisitiza elimu kuhusu haki za watoto ni muhimu na kuwa jamii inapaswa kuzingatia malezi bora ya watoto.
Alisema kuwa suala la malezi ni changamoto kubwa, na familia na jamii zinapaswa kufuatilia mienendo ya watoto wao shuleni na mitaani.
Asia alifafanua ,zoezi hilo litakuwa la siku tisa, ambapo watafika kwenye kata kumi na vitongoji 30 na litakamilika machi 5, 2025.
Ally Cleophace Adrian,Wakili kutoka Chama Cha Wanasheria (TLS) aliwataka ,wananchi kuandika wosia mapema ili kuepuka migogoro ya kifamilia inayozuka wakati wa ugawaji wa mali baada ya kifo cha mpendwa.
Ally alieleza, kumekuwepo na migogoro mingi ya mirathi kutokana na imani potofu ya jamii kwamba kuandika wosia ni kujitabiria kifo.
Sajenti Saida Hamis kutoka Dawati la Jinsia na Watoto, Polisi Chalinze, alitoa elimu kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia na jinsi ya kujilinda dhidi ya ukatili huo.
Saida alisema, watu wanaopitia ukatili ikiwemo matukio ya ubakaji, ulawiti wanapaswa kutoa taarifa kwa haraka kwa kupiga simu bure kupitia namba 116 na 112.
Ofisa Ustawi wa Jamii Chalinze, Atuganile Chisunga, alisisitiza umuhimu wa shule kuwa na masanduku ya maoni ili kuwasaidia wanafunzi kufichua vitendo viovu vya maadili.
Aliongeza kuwa ,kamati za MTAKUWA (Mifumo ya Tawala za Vijiji na Kata) zinapaswa kutekeleza wajibu wao kwa ukamilifu ili kuwasaidia watoto na vijana katika jamii.