NA VICTOR MASANGU,PWANI
SERIKALI mkoani Pwani imetangaza kuwa sherehe za uwashwaji rasmi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa zitafanyika Aprili 2 mwaka huu 2025 katika viwanja vya shirika la Elimu Kibaha.
Akizungumza na waandishi ofisini kwake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaji Abubakari Kunenge amesema kwamba Rais wa awamu ya sita Dkt.Samia Suluhu Hassan ameutewa Mkoa wa Pwani kuwa mwenyeji katika sherehe hizo.
Kunenge amebainishwa kwamba maandalizi yote kwa ajili ya sherehe hizo za uwashwaji wa Mwenge wa uhuru kitaifa yanaendelea vizuri na kwamba tukio hilo ni kubwa na la kihistoria.
“Tupo katika maandalizi kwa ajili ya tukio kubwa la uwashwaji wa mbio za Mwenge huo wa Uhuru kitaifa ambapo mkoa wetu tumepewa heshima kubwa kuwa ndio wenyeji “amesema Kunenge.
Kadhalika ameongeza kuwa sherehe hizo zitahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na mikoa jirani ikiwa pamoja na wageni wengine.
Alisema kuwa sherehe hizo za uzinduzi zitapambwa na matukio mengi yakiwemo ya halaiki na burudani nyingine za wasanii.
“Baada ya uzinduzi huo mwenge wa uhuru utakimbizwa katika Halmashauri tisa za mkoa huo ambapo utakagua, kutembelea na kuzibdua miradi mbalimbali ya maendeleo,”alisema Kunenge.
Aidha alisema kuwa kuwashwa mwenge wa uhuru hapa kwetu ni fursa kiuchumi kwa watu wa Pwani pia chachu ya maendeleo kwani wananchi watafanya biashara za chakula, malazi, usafiri, vinywaji na utalii.
Mkuu huyo aliwahimiza wananchi wote wa Mkoa wa Pwani kujitokeza kwa wingi na kutumia fursa hiyo katika suala zima la kukuza uchumi wao kupitia biashara mbali mbali