Na Mwamvua Mwinyi, Mkange-Chalinze
Feb 28,2025
Shule ya Msingi Mkange, iliyopo Chalinze, mkoani Pwani, inakabiliwa na changamoto kubwa ya uchakavu wa miundombinu, ambapo vyumba vya madarasa vitatu vimechakaa na madarasa mawili hayatumiki ili kuepuka hatari kwa wanafunzi.
Hali hii ilibainika wakati wa ziara ya maofisa kutoka Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya MAMA SAMIA,Chalinze na wizara ya sheria na katiba walipofika kutoa elimu kuhusu haki za watoto kwa wanafunzi.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Mkange, Maiko Hinjo, alieleza kuwa shule hiyo ni kongwe ilianzishwa mwaka 1953, na tangu wakati huo, juhudi za ukarabati wa mara kwa mara zimekuwa zikifanyika.
“Shule hii ina zaidi ya wanafunzi 1,000, huku madarasa sita yanayotumika “Kwa mfano,kuna darasa moja lina wanafunzi 150, jambo ambalo linachangia msongamano na upungufu wa madawati”
“Hali hii inafanya kuwa vigumu kwa wanafunzi kufuata mpangilio mzuri wa masomo, na kila darasa linapaswa kuwa na wanafunzi 45.” alieleza Hinjo.
Alifafanua kuwa uchakavu wa miundombinu unahusisha madarasa, nyumba za walimu, na pia ukosefu wa ofisi ya walimu.
Hinjo alisisitiza kuwa shule haina shift kwa wanafunzi ambapo wanafunzi wengi wanalazimika kusoma kwa msongamano kwa ajili ya upungufu wa madarasa.
Hata hivyo, aliongeza kuwa wamewasiliana na halmashauri, na tayari fedha zimeidhinishwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na kuboresha miundombinu ya shule hiyo.
Kadhalika, alieleza halmashauri imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo, na ujenzi umekamilika.
“Wazazi wamejizatiti kwa kuanzisha utaratibu wa nguvu kazi ili kujenga darasa moja, na ujenzi wa msingi utaanza hivi karibuni.” anaongeza Hinjo.
Asia Festus, Wakili na Mratibu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, alieleza kuwa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya MAMA SAMIA inaendelea kutembelea kata kumi na vitongoji 30 ndani ya Halmashauri ya Chalinze kutoa elimu kuhusu msaada wa kisheria kwa jamii.
Alieleza watoto wana haki ya kusikilizwa na kupata elimu katika mazingira bora, na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kutenga fedha katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu.
Ofisa elimu awali na msingi Chalinze, Miriam Kihiyo alipoulizwa kwa njia ya simu juu ya changamoto hizo alieleza, kuna hiyo changamoto maana shule nyingi ni kongwe ila wameshatoa taarifa kwenye mamlaka.
Shule ya Msingi Mkange, inafundisha wanafunzi 1,173 kwa walimu tisa, inahitaji kuangaliwa kwa jicho la tatu ili kuhakikisha mazingira bora ya kujifunzia kwa wanafunzi wake.