NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameweka jiwe la msingi ujenzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Ndaki ya Tiba (College of Medicine) Kampasi ya Mloganzila pamoja na kuzindua Mfuko wa Maendeleo wa Ali Hassan Mwinyi wa MUHAS ( Ali Hassan Mwinyi MUHAS Endowment Trust Fund – AHMMEF) ambao umelenga kusaidia maendeleo endelevu ya elimu na tafiti.
Akizungumza katika Kongamano maalum la kumuenzi Mkuu wa Kwanza wa Chuo MUHAS na Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Ali Hassan Mwinyi lililofanyika leo Februari 28, 2025, Kampasi ya Mloganzila , Dar es Salaam, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameupongeza uongozi wa MUHAS kwa kuandaa kongamano hilo pamoja na kuanzisha mfuko ambao utakusanya fedha kwa ajili ya kuendeleza kazi za chuo.
Dkt. Mwinyi amesema kuwa mfuko huo unakwenda kutoa fursa ya elimu, kufanya utafiti pamoja na kutoa huduma kwa jamii, huku akieleza kuwa kongamano hilo limeweza kuwapa nafasi ya kusikia namna chuo kilivyonufaika na mchango wa mkuu wa chuo Hayati Ali Hassan Mwinyi katika kipindi cha miaka 17.
Amesema kuwa Hayati Ali Hassan Mwinyi amekuwa na mchango mkubwa katika maeneo mbalimbali hasa ustawi wa MUHAS ikiwemo upanuzi wa miundombinu ya kufundishia katika kampasi ya mloganzila na kusaidia kuboresha huduma ya afya, elimu na utafiti.
“Nimefarijika kuona chuo kinafanya kongamano la kisayansi kila mwaka kwa ajili ya kumuenzi Hayati Ali Hassan Mwinyi, natambua kwamba makongamano haya yanawaleta pamoja wawakilikishi mbalimbali wasomi, wanasayansi, wanataaluma, washirika wa maendeleo, watenga sera pamoja na wadau wengine kwa ajili ya kujadili maendeleo” Dkt. Mwinyi.
Amesema kuwa kama familia wanashukuru kwa uwepo wao kwa ajili ya kumuenzi mzee Mwinyi ambaye alifanya kazi katika nafasi mkuu wa chuo MUHAS. Dkt. Mwinyi amehaidi kutoa ushirikiano kwa uongozi wa chuo hicho ikiwemo kuzifanyia kazi changamoto ya miundombinu ya barabara pamoja na kujenga hosteli za wanafunzi na kuzifikisha mahali husika kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa, Adolf Mkenda amesema kuwa matamanio ya serikali ni kuhakikisha eneo la Mloganzila linakuwa mji wa taaluma za afya ifikapo mwaka 2050.
Amesema kuwa ujenzi wa Ndaki ya Tiba chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa ajili ya kuongeza miundombinu ya kujifunzia na hosteli utakaokamilika Juni, 2026.
Profesa Mkenda amesema kuwa lengo ni kuongeza wataalamu wa afya ndani na nje ya Tanzania wenye uwezo wa kupambana na changamoto mbalimbali za afya kutokana na maendeleo ya teknolojia na mabadiliko ya tabia nchi.
“Wizara ya elimu ipo tayari kuchangia mfuko huo, hivyo kabla ya kwenda kuchangiwa na taasisi zingine pamoja na wadau ni vyema ukapita kwanza katika wizara ili iweze kuchangia kabla ya kwenda kuchangiwa na wengine” amesema Prof Mkenda.
Makamu Mkuu wa Chuo MUHAS Chuo Profesa Appolinary Kamuhabwa, amesema kuwa tayari wamekamilisha usajili wa Mfuko wa Maendeleo wa Ali Hassan Mwinyi wa MUHAS kwa ajili ya kuanza kupokea fedha kutoka kwa wadau wa maendeleo, wahitimu pamoja na watu binafsi.
Profesa Kamuhabwa amesema kuwa mfuko huo ni kwa ajili ya kutoa msaada wa kifedha wa kudumu kwa miradi bunifu, programu za kitaaluma na ustawi wa wanafunzi na wanataaluma ili kuhakikisha kuwa MUHAS inaendelea kuwa chuo bora cha elimu ya afya na sayansi shirikishi pamoja utoaji huduma za afya na utafiti nchini.
“Lengo ni kufikia matamanio ya hayati Ali Hassan Mwinyi ikiwemo kuhakikisha miundombinu ya chuo inaimarika, ndiyo maana leo tumeweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa ndaki ya tiba pamoja na kujenga hosteli za wanafunzi” amesema Profesa Kamuhabwa.
Katika kongamano hilo uongozi wa MUHAS ukikabidhi vazi rasmi la mkuu wa kwanza wa chuo kwa familia ya Hayati Ali Hassan Mwinyi ambalo amekuwa akilitumia kulivaa wakati wa mahafali wakati wa uhai wake.