Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeanza kutoa ruzuku kwenye miradi ya nishati ya gesi ya kupikia, majiko ya gesi na majiko ya umeme ikiwa ni utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwa kuhamasisha na kurahisisha upatikanaji wa nishati safi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa B. Nyanga, imesema kuwa
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo wakati wa uzinduzi rasmi wa Mradi wa Usambazaji wa Mitungi ya Gesi ya Kupikia 551,795 nchi nzima kwa bei ya ruzuku iliyofanyika katika Wilaya ya Muheza ambapo Rais Dkt. Samia ametoa mitungi ya gesi asilia kwa wawakilishi na wakazi wa Wilaya zote za Mkoa wa Tanga.
Mradi huo utahusisha usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia, majiko banifu 205,000 na miundombinu ya gesi asilia katika Mikoa ya Lindi na Pwani.
Aidha, Rais Dkt. Samia amesema Serikali itaendelea kutunga sera zitakazoimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa bei nafuu na kwa urahisi ili kuimarisha ustawi wa wananchi na kulinda mazingira.
Katika hatua nyingine, leo Rais Dkt. Samia amefungua rasmi kiwanda cha Saruji na Chokaa cha Maweni Limestone katika Jiji la Tanga, uwekezaji unaoendana na dhamira ya Serikali ya kurejesha hadhi ya Mkoa wa Tanga kama mkoa wa viwanda.
Rais Dkt. Samia amesema kuwa uamuzi wa kampuni ya Maweni Limestone kupanua uwekezaji wake nchini ni ishara ya imani ya wawekezaji kwa sera za uwekezaji, mazingira ya biashara na rasilimali watu nchini Tanzania.
Aidha, Rais Dkt. Samia ametumia fursa hiyo kukumbushia wajibu wa wawekezaji wote na wenye viwanda wote nchini kulipa kodi stahiki za Serikali Kuu na ushuru wa Halmashauri kwani ndio fedha zinazotegemewa kuwezesha maendeleo ya wananchi.
Vilevile, Rais Dkt. Samia ameweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Maji wa Tanga – Horohoro unaohusisha ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita 91.9.
Akizungumza na wananchi katika Stendi ya Mabasi Mkinga Rais Dkt. Samia amesema mradi huo utawahakikishia maji safi na salama wananchi takriban 57,000 katika Vijiji 37 katika Wilaya ya Mkinga na Wilaya ya Tanga.
Matukio hayo yamefanyika leo ikiwa ni siku ya tano ya ziara ya Rais Dkt. Samia katika Mkoa wa Tanga.
Kesho tarehe 28 Februari, 2025, Rais Dkt Samia anatarajia kuzungumza na wakazi wa Mkoa wa Tanga katika Mkutano wa Hadhara utakaofanyika katika Uwanja wa Mkwakwani katika Jiji la Tanga.