Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda amemtembelea Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abass ofisini kwake na kufanya mazungumzo na Kamati ya Ulinzi na Usalama Leo tarehe 27 Februari 2025.
Katika mazungumzo yao Jenerali Mkunda amempongeza Mkuu wa Mkoa pamoja na Kamati yaUlinzi na Usalama ya Mkoa huo kwa kuhakikisha kuwa hali ya Usalama katika eneo la mpaka wa Tanzania kwa upande wa Mkoa wa Ruvuma liko salama wakati wote.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mheshimiwa Kanali Ahmed Abass Ahmed amelishukuru JWTZ kwa namna linavyohakikisha Mkoa wa Ruvuma unakuwa salama wakati wote hali inayosababisha wananchi wa Mkoa huo na maeneo ya jirani kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu.Amemhakikishia kuwa uongozi wa Mkoa utaendelea kutoa ushirikiano kwa JWTZ katika mambo yote ambayo utahusishwa.
Kwa mujibu wa Msemaji wa JWTZ Kanali Gaudentius Ilonda,Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi yuko mkoani Ruvuma kwa ziara ya kikazi ambapo pamoja na mambo mengine atashiriki Sherehe za Kumbukumbu ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji inayofanyika leo tarehe 27 Februari 2025.