Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda amewaongoza maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na maeneo jirani katika Maadhimisho ya Miaka 120 ya Kumbukumbu ya Vita vya Majimaji yaliyofanyika tarehe 27 Februari 25 katika eneo la Makumbusho ya Vita vya Majimaji mjini Songea.
Katika hotuba yake Jenerali Mkunda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyotoa kipaumbele katika kuhifadhi Kumbukumbu muhimu za Mashujaa wa Tanzania waliopambana ili kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa salama.
Amewaomba wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na maeneo yote ambayo Vita vya Majimaji vilipiganwa kuendelea kutunza historia hii nzuri kwaajili ya urithi kwa vizazi vijavyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abass Ahmed amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Chifu Hangaya kwa namna anavyohamasisha utamaduni ili kutunza historia na kukuza utalii wa Tanzania.
Aidha amelishukuru JWTZ pamoja na kuwa na jukumu lake la msingi la kulinda mipaka ya nchi pia limekuwa linashiriki kutoa huduma za kijamii kama vile matibabu na elimu kupitia hospitali na Shule za JWTZ hali inayotafsiri kuwa kweli ni Jeshi la Wananchi.
Nae Chifu Mkuu wa kabila la Wangoni Emanuel Zulu Gama, amesema kuwa kitendo cha Serikali kuendelea kuhifadhi historia muhimu ya Ulinzi wa taifa kama vile Vita vya Majimaji kimesaidia kuwaenzi Mshujaa wetu na kurithisha taarifa hizi kutoka kizazi hadi kizazi.
Katika tukio hilo Jenerali Mkunda aliweka mkuki na ngao ,Mkuu wa Mkoa aliweka sime,Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea akiweka upinde na mshale na Chifu Gama akiweka shoka ikiwa ni ishara ya heshima kwa Mashujaa hao.Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi wa dini mbalimbali,vyama vya siasa, Machifu kutoka makabila mbalimbali kutoka Tanzania,Afrika ya Kusini na Malawi.
Maadhimisho hayo yamepambwa na gwaride rasmi la maombolezo lililoandaliwa na JWTZ,Maonesho ya Zana mbalimbali zilizotumika wakati wa Vita vya Majimaji pamoja na burudani mbalimbali ikiwa ni kuwaenzi Mshujaa wa Vita hivyo vilivyopiganwa Mwaka 1905.