************
Na Sixmund Begashe – Mwanza
Viongozi na watumishi katika ngazi mbalimbali za Serikali wameshauriwa kuungana kwa pamoja kushughulikia tatizo la mimea vamizi kupitia ripoti itakayotolewa na Wataalamu kwani tatizo hilo lisipotatuliwa kwa haraka athari zake zitakuwa kubwa hususani katika sekta ya Utalii ambapo ameeleza sekta ya Utalii inachangia asilimia 17 ya pato la taifa, asilimia 25 ya fedha za kigeni ambazo ni muhimu kwa ustawi wa uchumi wa nchi.
Wito huo umetolewa na Balozi wa Tanzania nchini Cuba Mhe. Humphrey Polepole katika kikao kazi cha hitimisho ya ziara ya timu ya Watafiti wa Mimea vamizi kutoka Jamhuri ya Cuba walioungana na Wataalamu wa Ikolojia kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii kilichofanyika katika Chuo cha Wanyamapori Pasiansi mkoani Mwanza ambapo amesema kupitia Wataalamu hao kuwa suluhu inakwenda kupatikana.
“Natoa rai kwa watumishi na viongozi wenzangu serikalini, Mhe, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuamini, ametupatia dhaman hizi ili tutatue kero na changamoto za wananchi wetu, mbuga zetu na hifadhi zetu. Utalii unachangia asilimia 17 ya pato la taifa, asilimia 25 ya fedha za kigeni ambazo ni muhimu kwa ustawi wa uchumi wetu, kuendelea kuwepo kwa mimea vamizi na kutochukua hatua sasa kunahatarisha zaidi fedha za kigeni zinazokuja nchini kwetu kupitia utalii. Ombi langu kwa viongozi wenzangu tukaifanyie kazi ripoti itakayotolewa kuleta suluhu ya tatizo hili.”-Aliongeza Mhe. Polepole
Mhe. Balozi Polepole mesema ziara ya Watafiti wa Mimea Vamizi kutoka Jamhuri ya Cuba inakwenda kuwa msaada wa kutafuta suluhu ya kudumu ya changamoto hiyo ambayo imekuwa ikihatarisha ustawi wa ikolojia ya hifadhi, Vyanzo vya Maji, Mazingira, Sekta ya Uvuvi, Kilimo na Usafirishaji.
“Leo tumehitimisha ziara ya Wataalamu kutoka Tanzania na Cuba ambao wamekuwa hapa kwa siku 10 na walikuwa wana kazi ya kutafuta suluhu ya kudumu ya mimea vamizi ambayo inayohatarisha ustawi wa ikolojia ya mbuga na hifadhi zetu hususan Ngorongoro, mbuga ya Serengeti lakini pia kwa pamoja Wataalamu hawa kwa pamoja walikwenda Ziwa Viktoria na wameona athari mbaya zinazoletwa na magugu maji ambayo ni hatari zaidi”- Alisema Mhe, Balozi Polepole.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Mazingira na Jiografia kutoka nchini Cuba Bw. Orlando Enrique ameeleza kuwa ziara hiyo waliohitimisha Mkoani Mwanza ni muhimu kwao hususani katika kuongeza wigo wa mahusiano baina yao na Tanzania pamoja na uelewa walioweza kujengeana na watafiti kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.
Akiwawakilisha kundi la Wataalamu kutoka Tanzania Mtafiti Mkuu kutoka TAWIRI Dkt. John Bukombe amesema ipo fursa katika Mimea Vamizi hivyo kupitia uelewa wa pamoja waliojengeana na tathmini waliyoifanya wataokoa Malisho ya Wanyamapori na mimea inayohitajika lakini pia wanaweza kutumia kuzalisha dawa zitokanazo na mimea kwa kuwatumia Wataalamu wa kutoka Cuba.
Ziara hiyo ya kihistoria ilihusisha watafiti kutoka nchini Cuba na wataalam kutoka taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii zikiwemo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, TANAPA, TAWIRI na TAFORI imehitimishwa rasmi jijini Mwanza kwa kufanyika kikao cha majumuisho kilichohusisha taasisi mbalimbali za Serikali.