Na Mwamvua Mwinyi
Februari 24, 2025
Ofisa Elimu Taaluma wa Mkoa wa Dar es Salaam, Eva Mosha, ametoa rai kwa wamiliki na walimu wa shule binafsi za awali na msingi kuimarisha ufanisi wa ufundishaji na kuboresha ubora wa elimu, ili kuinua taaluma katika shule zao.
Amesisitiza ,shule hizo zinapaswa kuongeza ubunifu na kujiendeleza kwa kupata mafunzo mbalimbali ya namna ya kuendesha shule zao, ili kuepuka changamoto za kushindwa kuendeleza shule au kukosa wanafunzi.
Mosha alitoa rai hiyo katika hafla ya kupongeza walimu na wamiliki wa shule binafsi za awali na msingi, ambazo zinatoa ada nafuu, waliopatiwa mafunzo ndani ya miaka mitatu kupitia mradi wa Opportunity International ,kwenye ukumbi wa Victoria uliopo Kimara Temboni, Dar es Salaam.
Mratibu wa Mradi wa Opportunity International Tanzania (HES Tanzania), Oliver Kapaya, alieleza kuwa mradi huo ulianza mwaka 2018 na umefanikiwa kuhusisha shule 101 katika kipindi cha miaka mitatu.
Alieleza, shule 74 zilipata mafunzo na kufuzu kwa kipindi cha miaka minne na shule 15 zimefanikiwa kupata tuzo za kutambua ufanisi wao huku, shule nane zimetunukiwa tuzo kwa utendaji bora.
Violet Oketch, mratibu wa Mradi wa Opportunity International Afrika (HES Africa), alieleza mradi huu unatekelezwa katika nchi nane za Afrika, ikiwa ni pamoja na Tanzania, Rwanda, Zambia, Ghana, DRC Congo, Uganda, Kenya, na Nigeria.
Violet Oketch alishukuru serikali ya awamu ya sita kwa ushirikiano wake na wawekezaji na wafadhili mbalimbali katika sekta ya elimu.
Brayson Ephata Maleko, Ofisa Elimu Vifaa na Takwimu Temeke, alisema mradi huo umehusisha shule za awali na msingi, namna ya kuendesha shule kwa ufanisi, kupanga mipango, na kusimamia rasilimali fedha.