Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Februari 24, 2025
Sheikh wa Mkoa wa Pwani, Hamis Mtupa, ameiangukia Serikali kuiomba kufanyia maboresho suala la cheti cha ndoa kwa dini ya Kiislamu ili kiweze kutambulika kisheria.
Kwa mujibu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), cheti cha ndoa cha dini hakitoshi kukutambulisha kama mke na mume inapofika kwenye masuala ya kisheria.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria ya MAMA SAMIA (Samia Legal Aid) mnamo Februari 24, 2025, katika Mailmoja, Kibaha, Mtupa alieleza kuwa cheti hicho kinatambulika na BAKWATA pekee, jambo ambalo linazua usumbufu kwa waumini wa dini hiyo.
“Ili ndoa itambulike kisheria, lazima isajiliwe na wakala wa Serikali na kupewa cheti cha ndoa cha Serikali,” alisisitiza Mtupa.
Akizindua kampeni hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, aliwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi ili kupata msaada wa kisheria kuhusu changamoto mbalimbali kama vile ndoa, mirathi, ukatili wa kijinsia, na migogoro ya ardhi.
Alisema hatua hiyo ni sehemu ya kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kutatua changamoto za kisheria kwa wananchi.
Akitoa salamu za Wizara ya Katiba na Sheria, Naibu Waziri Jumanne Sagini alisema kampeni hii ilianza mkoani Mwanza tarehe 19 Februari, na baadae kuanzishwa mkoani Lindi tarehe 24 Februari. Kampeni pia imezinduliwa katika mikoa ya Mbeya na Pwani, na itazinduliwa mkoani Rukwa tarehe 25 Februari, 2025.
Alieleza kuwa Wizara imejipanga kuhakikisha kuwa ifikapo Mei, 2025, kampeni itakuwa imetekelezwa kikamilifu katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.
“Kampeni hii imeleta unafuu mkubwa kwa wananchi katika kuifikia haki kwani uelewa katika masuala ya kisheria umeongezeka, Hii inajidhihirisha kupitia idadi ya wananchi inavyozidi kuongezeka katika kuitafuta haki na kupata ushauri wa kisheria,” alisema Sagini.
Alibainisha kuwa Wizara ya Katiba na Sheria inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanaifikia haki kwa wakati na kwa ufanisi.
Sagini alisema, Wizara imejipanga kwa dhati katika utekelezaji wa kampeni na mara baada ya uzinduzi wataanza kutoa huduma kuanzia tarehe 25 Februari hadi 5 Machi, 2025.
Naye Mwanaidi Ali Khamis (Mb), Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, aliwataka wananchi kufika kwenye vyombo vya Sheria pindi wanapokutana na changamoto yoyote ya kisheria.