Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, akizungumza wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani, Februari 24, 2024.
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Ahmad Abdallah Akielezea mafanikio ya Shirika hilo kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Msajili wa Hazina Bw.Nehemiah Mchechu kufungua kikao hicho.
…………………
Na John Bukuku, Pwani
Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, amelielekeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuongeza kiwango cha gawio kwa Serikali hadi kufikia shilingi bilioni 10. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutekeleza miradi kwa ubunifu ili kutumia rasilimali za shirika kwa ufanisi, jambo ambalo litasaidia kupunguza changamoto ya uhitaji wa nyumba nchini.
Akizungumza leo Februari 24, 2025, wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa NHC katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani, Mchechu amesema kuwa NHC ni moja ya mashirika ambayo Serikali inajivunia kutokana na utendaji wake mzuri katika utekelezaji wa miradi.
Amesema amefurahishwa na juhudi za wafanyakazi wa NHC, hasa kwa kuwa na mpango wa kuongeza mchango wao kwa mfuko mkuu wa Serikali kutoka shilingi bilioni mbili hadi kufikia bilioni sita, mbali na kodi na makusanyo ya Serikali.
“Ni muhimu kwa wafanyakazi kuwa na umoja, mshikamano, ubunifu na upendo, huku mkiepuka majungu katika utendaji kazi wenu,” amesema Mchechu.
Aidha, ameeleza kuwa miradi inayotekelezwa na NHC katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mtwara, Lindi, na Iringa inakaribia kukamilika, na italeta manufaa makubwa kwa Taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Ahmad Abdallah, amesema kuwa shirika limeendelea kufanya maboresho makubwa ili kuleta matokeo chanya katika utekelezaji wa miradi.
Amefafanua kuwa mipango mizuri ya NHC imefanikiwa kuleta maendeleo katika miradi yake, huku thamani ya shirika hilo ikiongezeka kutoka shilingi trilioni 5.04 mwaka 2024 hadi kufikia trilioni 5.5 mwaka 2025.
Abdallah pia amesema kuwa NHC hulipa kodi ya wastani wa shilingi bilioni 30 kila mwaka, na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi kwa wakati.