Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Profesa Appolinary Kamuhabwa akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 24, 2025 jijini Dar es Salaam kuhusu kongamano maalum la kumuenzi Mkuu wa kwanza wa Chuo hicho na Rais wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Ali Hassan Mwinyi litakalofanyika Februari 28, 2025 katika Kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu, Kampasi ya Mloganzila.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Profesa Appolinary Kamuhabwa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Kongamano la kongamano maalum la kumuenzi Mkuu wa kwanza wa Chuo MUHAS Profesa Raphael Sangeda (wa kwanza kukulia) na Mkurugenzi wa Utafiti, Machapisho na Ubunifu MUHAS Profesa Nahya Salm Masoud wakati wakizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
…..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kinatarajiwa kufanya kongamano maalum la kumuenzi Mkuu wa Kwanza wa Chuo hicho na Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Ali Hassan Mwinyi litakalofanyika Februari 28, 2025 katika Kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu, Kampasi ya Mloganzila.
Katika kongamano hilo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, pamoja na wageni mashuhuri wakiwemo viongozi wa serikali, wanazuoni, wataalamu wa afya, wahisani, wadau wa elimu wanatarajiwa kushiriki.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 24, 2025 Jijini Dar es Salaam, Makamu Mkuu wa Chuo MUHAS Profesa Appolinary Kamuhabwa, amesema kuwa lengo la kongamano ni kuthamini mchango mkubwa wa Hayati Ali Hassan Mwinyi katika maendeleo ya elimu, afya, na ustawi wa jamii kwa ujumla.
Profesa Kamuhabwa, amesema kuwa katika kongamano hilo kutakuwa na matukio mbalimbali ikiwemo uzinduzi wa Mfuko wa Maendeleo wa Ali Hassan Mwinyi wa MUHAS (Ali Hassan Mwinyi MUHAS Endowment Trust Fund – AHMMEF) ambao umelenga kusaidia maendeleo endelevu ya elimu na tafiti chuoni.
“Mfuko huu utatoa msaada wa kifedha wa kudumu kwa miradi bunifu, programu za kitaaluma, na ustawi wa wanafunzi na wanataaluma, lengo ni kuhakikisha MUHAS inaendelea kuwa Chuo bora cha elimu ya afya na sayansi shirikishi, utoaji huduma za afya na utafiti nchini Tanzania na kwingineko” amesema Profesa Kamuhabwa.
Profesa Kamuhabwa amesema kuwa pia watafanya uzinduzi wa Kongamano la kila Mwaka la Ali Hassan Mwinyi ambapo litakuwa jukwaa la kipekee linalowaleta pamoja wataalamu wa sekta ya afya na elimu kwa ajili ya kujadili masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya sekta na mustakabali wake.
Ameeleza kuwa lengo ni kukumbuka na kuthamini mchango wa mkuu wa kwanza wa chuo cha MUHAS katika masuala mbalimbali ikiwemo maendeleo ya chuo, mijadala yenye lengo la kusaidia kuimarisha mifumo ya afya na elimu nchini.
“Pia kutakuwa na tukio la kurejesha vazi rasmi la mkuu wa kwanza wa chuo kwa familia ya Hayati Ali Hassan Mwinyi, ambalo amekuwa akilitumia kulivaa wakati wa Mahafali hapa Chuoni” amesema Profesa Kamuhabwa.
Amefafanua kuwa kutakuwa maonesho ya afya na elimu kwa ajili ya kuonesha mafanikio makubwa katika sekta ya afya na elimu ikiwemo utafiti mpya, ubunifu wa kiteknolojia na juhudi zinazofanywa na MUHAS katika kuboresha huduma bora za afya nchini.
Amesema kuwa washiriki wa kongamano watajionea miradi inayoendelea na kushuhudia jinsi teknolojia mpya inavyoboresha utoaji wa huduma za afya na mafunzo kwa wataalamu wa afya kwa siku zijazo, na pia watapata huduma za bure kupima afya zao.
Profesa Kamuhabwa kutakuwa na wekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha Tiba katika kuimarisha zaidi mazingira ya mafunzo, huduma za afya na kufanya tafiti.
“Tukio hili litatumika kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Ndaki ya Tiba (College of Medicine) kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) katika Kampasi ya Mloganzila, mradi huu ni hatua kubwa kuelekea kupanua miundombinu ya Chuo na hivyo kuongeza udahili wa wanafunzi na kuboresha ubora wa mafunzo kwa wanafunzi” amesema Profesa Kamuhabwa.
Amesema kuwa katika kufanikisha kongamano hilo, kutakuwa na kambi maalum ya wahudumu wa afya kuanzia Februari 26-27, 2025 ikiwa ni sehemu ya maandalizi.
Amesema kuwa kambi hiyo itakuwa kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni katika Kampasi ya Mloganzila, huku akitoa wito kwa wananchi kujitokeza kupata huduma za uchunguzi wa awali kwa magonjwa mbalimbali ikiwemo Macho , Masikio, Pua na Koo Kinywa na Meno, Saratani ya Matiti na Shingo ya Kizazi, Homa ya Ini, Tezi Dume kwa kipimo cha damu.
“Pia kutatolewa elimu kuhusu madhara ya matumizi ya dawa na usugu wa dawa mwilini, magonjwa ya kuambukiza, utengenezaji na ukarabati wa vifaa tiba, uchakataji wa taarifa za afya kwa kutumia akili mnemba pamoja na lishe” amesema Profesa Kamuhabwa.