







Zafa hiyo ilijumuisha waumini kutoka maeneo mbalimbali ya jiji, na yalianza kutoka Msikiti wa Raudhwa uliopo Mtaa wa Lumumba, yakipitia barabara kuu za Nyerere, Nkurumah, Uhuru, Makongoro, Kenyatta na Posta kabla ya kufika Uwanja wa Nyamagana, ambapo walipokelewa na Sheikh Haruna Kichwabuta, ambaye ni Mwenyekiti wa Masheikh Tanzania na Sheikh wa Mkoa wa Kagera.
Sheikh Kichwabuta akizungumza baada ya kupokea Zafa hiyo amehimiza umuhimu wa kuukaribisha mwezi wa Ramadhani kwa imani thabiti, akifafanua kwamba ni mwezi bora kuliko miezi mingine, ambapo Qur’ani ilishushwa na milango ya pepo hufunguliwa.
Amesma Zafa hiyo ya kidini ni sehemu ya sherehe za kiimani zinazofanyika kila mwaka ili kumkaribisha mwezi wa Ramadhani, kipindi cha ibada na kujitakasa ambapo waumini wa Kiislamu wanatambua Ramadhani ni wa baraka na msamaha, na maadhimisho haya yanatoa fursa ya kuimarisha imani na kushirikiana kama jamii ya kiroho
“Mwezi wa Ramadhani ni mwezi bora kuliko miezi mingine, ni mwezi wa baraka na ni wakati ambapo Qur’ani ilishushwa.Milango ya pepo hufunguliwa na shetani hufungwa,” amesisitiza Sheikh Kichwabuta.
Ameongeza kuwa mwezi huu ni muhimu katika maisha ya kila Muislamu na ni wakati wa kujitafakari na kufanya ibada kwa wingi.
“Niwashukuru Jumuiya ya Kuendeleza Qu’ran na Sunna(JUQUSUTA) ya Mtume Muhammad S.A.W ambao ni wasimamizi wa Maulid katia taifa hili. Zafa hii si ya kwanza, ilianzia Madina na tunajitahidi kumhudhurisha Mtume,”amesema.
Sheikh Kichabuta amesema mwezi wa Ramadhan ni mwezi bora kuliko miezi mingine, yako mambo mengi ambayo hayatokei katika 11.
Sheikh Kichwabuta pia amekumbusha waumini umuhimu wa umoja na mshikamano katika kipindi hiki huku akiwahimiza waumini kukusanyika usiku kwa ajili ya kujifunza na kuelewa mambo muhimu yanayotarajiwa kufanyika nchini, ikiwa ni pamoja na Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
“Kauli mbiu yetu ni ‘Kuna Maisha baada ya Uchaguzi; Linda Amani, Chagua kwa Hekima.’Tufanye juhudi za kuhakikisha kuwa tunaishi kwa amani na utulivu, ili kuleta maendeleo ya kweli,” amesema.
Kupitia maandamano haya ya Zafa, waumini watumie fursa hii kuleta umoja na mshikamano, huku wakikumbuka umuhimu wa maisha baada ya uchaguzi na kutunza amani kwani ina maana kubwa katika kipindi cha uchaguzi,ikisisitiza kuwa umoja na amani vinahitajika kwa jamii zote ili kuleta maendeleo endelevu.