Na. Jacob Kasiri – Iringa.
Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) leo Februari 22, 2025 amezindua Safari za Ndege za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kutoka Dar es Salaam hadi Iringa (DAR – IR). Katika uzinduzi huo TANAPA kupitia Hifadhi ya Taifa Ruaha wameshiriki kama wanufaika na wadau wakubwa wa Uwanja huo kutokana na watalii mbalimbali kutokea jiji hilo la kibiashara nchini Tanzania kurahisishiwa usafiri.
Akiwa katika tukio hilo Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Abel Mtui ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha alisema, “Ujio wa Ndege za “ATCL” katika Uwanja wa ndege wa Nduli Mkoani Iringa utaongeza idadi ya watalii ndani ya hifadhi hiyo ya pili kwa ukubwa nchini Tanzania.”
Vilevile, Kamishna Mtui aliongeza kuwa awali walikuwa wakipata watalii waliokuwa wakishukia Uwanja wa Kimataifa wa Songwe uliopo jijini Mbeya na kusafiri kwa magari zaidi ya kilometa 400 hadi ndani ya hifadhi hiyo, hivyo Uzinduzi wa Safari za Ndege ATCL mjini Iringa utawapunguzia adha watalii badala ya kutumia km zaidi ya 400 sasa watatumia kilometa 128 tu na kuanza kufanya utalii ndani ya Hifadhi hiyo.
Aidha, Kamishna Abel Mtui alipata wasaa wa kuongea na Mkurugenzi wa ATCL Eng. Peter Ulanga kuhusu kuutumia Uwanja Mpya unaojengwa ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha (Kiganga) kipindi utakapokamilika ili kuongeza kasi ya ukuaji wa utalii na kuongeza mapato nchini.