Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aanatarajiww kuwa mgeni rasmi katika hafla muhimu ya uwekaji jiwe la msingi katika ujenzi wa Bwawa la Mkomazi na utiaji saini wa mikataba miwili ya ujenzi wa Skimu za Mkomazi na Chekelei wilayani Korogwe, mkoani Tanga Februari 24, 2025,
Mradi wa Mkomazi ni wa kihistoria, kwani ulianzishwa zaidi ya miaka 50 iliyopita lakini utekelezaji wake umekuwa ukisuasua kwa muda mrefu. Hata hivyo, chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, fedha zimepatikana kwa ajili ya kutekeleza mradi huu, ambao unatarajiwa kuwanufaisha wananchi zaidi ya 20,000 kutoka kata saba za Mkomazi, Mkumbara, Mazinde, Mombo, Chekelei, Makuyuni, na Magila Gereza.
Mradi wa Mkomazi unakadiriwa kugharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 18 na utahudumia vijiji 28 vilivyopo katika kata hizo. Mradi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 2025. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa tuta la udongo la kuzuia maji, ujenzi wa barabara kuelekea eneo la mradi, na ujenzi wa ofisi ya meneja wa mradi.
Katika hafla hiyo, Rais Samia pia atashuhudia utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa Skimu ya Mkomazi yenye jumla ya hekta 9,000, ambayo itahudumia kata hizo na vijiji 28 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 48.3. Aidha, Rais atashuhudia utiaji saini wa mkataba wa mradi wa Chekelei, ambao unahusisha ujenzi wa bwawa na skimu yenye ukubwa wa hekta 1,049, ambayo itawanufaisha wananchi kutoka vijiji vinne vya Madala, Madumu, Chekelei, na Chepete kwa gharama ya Shilingi Bilioni 31.2.
Tunaamini kuwa miradi hii itachochea maendeleo na kuboresha maisha ya wakazi wa Korogwe na maeneo jirani. Tunawashukuru wote kwa ushirikiano na tunawaomba waendelee kushiriki katika juhudi hizi za maendeleo kupitia kilimo cha umwagiliaji.