Timu ya riadha ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki – Nje Jogging imeshiriki mashindano ya Mbio za Kimataifa za Kilimanjaro (Kilimanjaro International Marathon 2025) na kujinyakulia medali mjini Moshi, Kilimanjaro Februari 23, 2025
Timu hiyo yenye jumla ya wanariadha 21 imeongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo.
Katika mbio hizo, wanariadha 13 walishiriki mbio za Kilometa tano (05) – (Fun run) na wengine 8 wakiongozwa na Balozi Shelukindo walishiriki mbio za umbali wa kilometa 21 (Yas half Marathon).
Akizungumza mara baaada ya kushiriki mbio hizo, Balozi Shelukindo amesema Wizara imeshiriki ili kuunga mkono Kili Marathon ambayo ni moja ya jukwaa la kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana mkoani Kilimanjaro ikiwa ni pamoja na Mlima Kilimanjaro na nchi nzima kwa ujumla.
Aidha, Balozi Shelukindo amewapongeza Nje Jogging kwa kuwa imara na kuweza kufanikiwa kukusanya medali 8 kwenye mashindano hayo, vilevile ametoa rai kwa wanamichezo wa Nje Sport kuendelea kujipanga na michezo iliyopo mbele yao kwa kuendelea kufanya mazoezi.
Pamoja na mambo mengine Balozi Shelukindo ametoa pongezi kwa waandaaji wa mashindano hayo ambayo yameendelea kujizolea umaarufu mkubwa nchini na hata nchi jirani.
“Maandalizi yamekuwa mazuri zaidi kulinganisha na mwaka uliopita uliopelekea kuongezeka kwa idadi ya washiriki na kufukia 20,000″, Balozi Shelukindo alisema.
Mgeni rasmi katika mbio hizo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Mashaka Biteko (Mb.) amewapongeza waandaaji wa mbio hizo pamoja na wadhamini na mdhamini mkuu Kilimanjaro Primier amekuwa akifanya hivyo kwa miaka 22 ambapo amedhamini kilometa 42, Kampuni ya Yasi imedhamini kilometa 21 na kampuni ya CRDB imedhamini Kilometa 5.