Mwenyekiti wa Baraza la vijana wa Chadema mkoa wa Rukwa Benjamin Mizengo wakati akimkabidhi mkuu wa kituo msaada
……………….
Na Neema Mtuka ,Sumbawanga Rukwa
Katika kuendelea kuigusa na kurudisha kwa jamii baraza la vijana wa chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema (BAVICHA) Mkoa wa Rukwa kimetoa msaada katika kituo cha kulelea watoto yatima cha mtakatifu Martine De Poles kilichopo Katandala.
Mwenyekiti wa baraza la vijana wa chama cha demokrasia na maendeleo chadema BAVICHA mkoa wa Rukwa Benjamini Mizengo amesema wametoa msaada huo kupitia kituo cha mtakatifu Martine DE Poles kilichopo katika kata ya Katandala Manispaa ya Sumbawanga wanapolelewa watoto hao yatima.
Mizengo amesema wao kama vijana wamejichanga na kukusanya msaada huo kutokana na nguvu zao na wamenunua vyakula, sabuni, mafuta na nishati ya kupikia kwa ajili ya watoto hao yatima na kufurahi nao pamoja.
Amesema baraza hilo lina utaratibu wa kusaidia jamii kwa kile wanachokipata kupitia shughuli na kazi zao wanazozifanya kwa ajili ya vipato vyao.
“Fedha za kununua mahitaji yote haya wanachama wamejitolea mifukoni mwao siyo kwenye mfuko wetu ni wale tulioguswa na kujitolea,” amesema Mizengo.
Mkuu shirika la masista wa malkia wa afrika ambaye pia ni mlezi wa watoto kituoni hapo St Agnes Kulyao amewapongeza BAVICHA kwa majitoleo yao na kusaidia watoto hao yatima katika kituo chao.
Kulyao amesema kitendo kilichofanywa na BAVICHA kinapaswa kuigwa na vyama vingine katika kusaidia wahitaji.
Awali akisoma taarifa fupi ya kituo hicho St Kulyao amesema kituo kina jumla ya watoto 31 ,19 ni wavulana na 12 ni wasichana pia wanalea watoto wa changa ambao wazazi wao walifariki pindi wanapojifungu .
Mmoja kati ya walezi wa kituo hicho Anna Simfukwe amewashukuru vijana hao kwa kutoa msaada kwa watoto hao yatima kwa kuwa wanapitia changamoto nyingi ikiwemo matibabu ya watoto hao.
“Tunamshukuru Mungu kwa neema yake kwani watoto hawa wamekuwa marafiki kwetu na tunawasaidia kwa moyo mmoja, tunawapongeza nanyi kwa kuja kuwasalimia watoto hawa,” amesema Simfukwe.