Madiwani na wenyeviti wa mitaa na vijiji Wilayani Biharamulo Mkoani Kagera wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kupatiwa Mafunzo kuhusu Ugonjwa wa Marburg.
Yasin Mwinory Afisa Afya Mkoa wa Kagera akitoa Mafunzo kuhusu ugonjwa wa Marburg kwa Madiwani na wenyeviti wa wa mitaa na vijiji.
Na. Elimu ya Afya kwa Umma.
Madiwani na baadhi ya wenye Viti wa Vijiji na Mitaa Wilaya ya Biharamulo Mkoani Kagera wamepatiwa Mafunzo namna ya kukabiliana na ugonjwa wa Marburg.
Akitoa Mafunzo hayo, Afisa Afya Mkoa wa Kagera Yasin Mwinory amewakumbusha viongozi hao kuwa mabalozi kwa wananchi katika kukabiliana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuepuka kuyatumia matunda yaliyokwaruzwa na wanyamapori kama vile maembe.
“Ukikuta embe limekwaruzwakwaruzwa na mnyama achana nalo maana huwezi kujua aliyekula hilo tunda ana Virusi vya Marburg au la”amesema.
Kwa Upande wake, Mratibu wa Elimu ya Afya Halmashauri ya Wilaya Biharamulo Veronica Joseph amesisitiza kuacha kusalimiana kwa kushikana mikono ni muhimu kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni na kupiga 199 bure .
“Ni vyema kuacha kusalimiana kwa kushikana mikono na niwaombe mkawe mabalozi kuiasa Jamii kujenga mazoea ya kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni”amesema.
Mafunzo hayo yameratibiwa na Wizara ya Afya, Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani(UNICEF) TIP ambao ni Mtandao wa Dini mbalimbali na Washirika wa Mtandao huo ambao ni BAKWATA, TEC,CCT, na Ofisi ya Mufti Zanzibar huku wadau wengine kama vile Afrika CDC wakishiriki katika Mafunzo hayo ambapo jumla ya viongozi 94 wamenufaika na Mafunzo hayo.
Kwa Upande wao baadhi ya Madiwani walioshiriki Mafunzo hayo wamesema watakuwa mabalozi katika Utoaji wa Elimu ya Afya kuhusu Ugonjwa wa Marburg huku wakiishukuru Serikali kwa kuweka jitihada kubwa katika mapambano ya Marburg.
Ikumbukwe kuwa unaweza kujikinga na ugonjwa wa Marburg kwa; Kuepuka kugusana na mtu mwingine mfano kusalimiana kwa kushikana mikono,kukumbatiana au kubusiana. Kuepuka kugusa majimaji ya mwili wa mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Marburg.
Kuepuka kugusa vitu kama vile vyombo, matandiko, magodoro vilivyotumiwa na mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Marburg. Kuepuka kuchangia vitu chenye ncha kali na mtu mwenye Maambukizi . Kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni mara kwa mara.