Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wamehimizwa kujitokeza na kuonesha umahiri wao kwa jamii na taifa kwa ujumla, sambamba na kueleza mchango wao kupitia tafiti mbalimbali wanazofanya.
Akizungumza katika mfululizo wa mihadhara ya wanataaluma wa SUA, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma wa SUA (SUASA), Dkt. Kassim Mussa, amesema lengo la mihadhara hiyo ni kujua wanataaluma waliorudi kutoka masomoni wamefanya nini, maeneo yao ya ubobezi, na namna wanavyoweza kusaidia jamii kupitia tafiti zao.
Amebainisha kuwa kupitia mihadhara hii, wanataaluma wataweza kufahamiana zaidi na kuelewa maeneo yao ya umahiri, hivyo kurahisisha mchakato wa kushirikiana katika kazi mbalimbali chuoni hapo.
“Mwanataaluma anafahamika kwa ufanisi na umahiri wake. Hatuwezi kutambua uwezo wao bila kuwapa fursa ya kuwasilisha tafiti na kazi zao. Hii ndiyo sababu tunafanya mfululizo wa mihadhara hii, tukishirikiana na Ofisi ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma), ambayo imeahidi kutoa ushirikiano wa karibu,” amesema Dkt. Mussa.
Kwa upande wake, mmoja wa washiriki wa muhadhara huo, Bi. Jenipher Tairo, Mhadhiri Msaidizi kutoka Idara ya Mimea Vipando na Mazao ya Bustani SUA, amepongeza uongozi wa chuo kwa kuanzisha mihadhara hiyo.
“Mihadhara hii ni muhimu sana kwa sababu inatupa fursa ya kujifunza kutoka kwa wengine, kujua matokeo ya tafiti zetu na namna zinavyoweza kusaidia jamii na taifa kwa ujumla. Tunahamasisha wanataaluma kujitokeza kushiriki kwa wingi ili kunufaika na fursa hii,” amesema Bi. Tairo.
Ameongeza kuwa uendelevu wa mihadhara hiyo utakuwa na manufaa makubwa kwa wanataaluma wa SUA na jamii kwa ujumla, kwani itasaidia kueneza matokeo ya tafiti mbalimbali zinazofanywa chuoni hapo.