

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Misungwi, Emmanuel Masangwa,amesema mazingira bora na wezeshi yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa wawekezaji wa nje na ndani ya nchi (wazawa),yatasaidia kukuza uchumi wa wilaya hiyo na taifa kwa ujumla.
Alitoa kauli hiyo jana,katika Kijiji cha Usagara wilayania Misungwi,wakati akizindua kituo cha Mafuta cha Fulano Petrol Oil kuwa,kitachochea maendeleo ya uchumi wa wilaya hiyo.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,imeweka mazingira bora na wezeshi kwa wafanyabishara wakubwa na wadogo hasa wazawa kukua kibiashara na kuongeza mchango katika ukuaji wa uchumi wa nchi ikiwemo Wilaya ya Misungwi.
“Serikali ya CCM imetoa fursa na imeweka miundombinu wezeshi kwa wafanyabiashara (wawekezaji) wazawa wazitumie fursa zilizopo Misungwi ili kuweza kukua kiuchumi,tunatamani kuona maendeleo kupitia biashara,tunampongeza Fulano kwa uwekezaji huo,tutaendelea kumuunga mkono na vijana wetu watapata ajira,”alisema Masangwa.
Alisema serikali ya awamu ya sita inaendelea kushirikiana na sekta binafsi kwa kuimarisha mazingira ya kufanya biashara, hivyo wawekezaji wengine wajitokeze na kuwekeza Misungwi bado kuna maeneo ya kutosha.
“Huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo barabara unaona zimeboreshwa,changamoto haziwe kwisha mara moja hata ya maji inaendelea kufanyiwa kazi na serikali.Uwekezaji huu umetupa heshima na naamini utakuwa na tija kwa wana Usagara na Misungwi kwa ujumla,niwaombe wadau wengine waje kuwekeza na tunawakaribisha sana,”alisema Mwenyekiti huyo wa CCM.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fulano Petrol Oil, Stepheno Fulano,alisema Rais Dk.Samia kwa kufungua fursa za biashara kwa wawekezaji wan je wakiwemo wazawa kupitia sera nzuri za serikali anayoiongoza,kumemsukuma kuwekeza katika biashara ya nishati ya mafuta.
Alisema kuwa,serikali kwa kutanua wigo kwa wawekezaji wa nje wakiwemo wa ndani ya nchi,malengo yake makubwa ni kukua kiuchumi na kujitanua zaidi kibiashara,kutoa ajira kwa wananchi,huduma kwa jamii na kupunguza changamoto za kijamii.
Fulano alisema Rais Samia anatamani Watanzania wawe wafanyabiashara wakubwa,hivyo ndoto yake (Fulano) kupitia uwekezaji fursa za ajira zimefunguka pamoja huduma za jamii,amejitoa kuwahudumia wananchi kwa huduma zenye ubora na atafanya kwa ubora zaidi.
“Dk. Samia, ni Rais wa pekee mwenye maono makubwa,wengi hawakumwelewa sasa wameanza kumwelewa.Watanzania wana imani naye na wanampenda,amewafikia na kutatua changamoto nyingi kwa muda mfupi,hivyo katika uchaguzi mkuu atashinda kwa asilimia 98,”alisema na kuongeza;
“Rais Samia ana matamanio Watanzania wawe wawekezaji wakubwa,binafsi nimevutiwa na sera za nchi yangu kufanya uwekezaji huu na hivyo nimefungua fursa za ajira na huduma za kijamii.”
Fulano ambaye pia anajihusisha na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali alisema uwekezaji aliofanya ni mwanzo mwema kupitia sera za Mama (Rais Samia Suluhu Hassan),alitoa wito kwa wadau mbalimbali kufika Fulano Petrol Oil kwa huduma na ushauri.
Awali Paroko wa Parokia ya Ilemela, Padri Evarist Shigi katika mahubiri yake wakati wa ufunguzi wa Kituo cha Fulano Petrol Oil alisema,Mungu alituweka juu ya kazi ya mikono yake na kutuagiza kufanya kazi halali ili kutafuta riziki na kipato.
Amlishukuru Fulano kwa kujitoa kuboresha maisha ya jamii ya Misungwi kutokana na biashara ya kuuza nishati ya mafuta.