Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango
akifanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania Mhe. Eunju
Ahn, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 19
Februari 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango
akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania Mhe.
Eunju Ahn mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani
Dodoma leo tarehe 19 Februari 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango
akiagana Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania Mhe. Eunju Ahn mara baada
ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 19
Februari 2025.
…..
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango
amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania
Mhe. Eunju Ahn, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo
tarehe 19 Februari 2025.
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amesema Tanzania inathamini na
imedhamiria kuimarisha ushirikiano na Jamhuri ya Korea ulioanza tangu mwaka
1992 ambao unachagiza maendeleo katika sekta mbalimbali nchini. Ameipongeza
Jamhuri ya Korea kwa kuiunga mkono Tanzania katika sekta ya Elimu, Miundombinu,
TEHAMA, Afya, Kilimo, Viwanda na Nishati.
Amesema makubaliano ya ushirikiano baina ya Tanzania na Korea katika madini ya
kimkakati yataleta manufaa mengi zaidi kwa kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na
madini mengi ambayo yanaenda sambamba na mwelekeo wa dunia ya sasa ambayo
inajikita katika uchumi wa teknolojia za kijani.
Aidha Makamu wa Rais amemueleza Balozi wa Jamhuri ya Korea umuhimu wa
kuongeza kiwango cha ufanyaji biashara baina ya Tanzania na Korea yenye manufaa
kwa pande zote mbili. Amesema ni muhimu wawekezaji na wafanyabiashara wa
Korea kutembelea Tanzania mara kwa mara ili kujionea fursa zilizopo na kuwekeza
nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo viwanda. Amesema uongezaji wa thamani
kwa malighafi hapa hapa nchini utachochea biashara, uhamishaji teknolojia pamoja
ongezeko la ajira kwa wananchi wa Tanzania.
Pia Makamu wa Rais amesema Tanzania ipo tayari kushirikiana na Jamhuri ya Korea
katika kubadilishana wafanyakazi, ambapo amemsihi Balozi huyo kuwezesha
mchakato wa kujiunga katika Mfumo wa Vibali vya Ajira (EPS) ili wafanyakazi wa
Tanzania waweze kuingia katika soko la ajira la Korea na kufanya kazi katika sekta
mbalimbali kama vile ujenzi wa meli, sekta ya viwanda na kilimo cha kisasa.
Halikadhalika amesema ushirikiano unahitajika katika Elimu na kuwajengea uwezo
wataalamu wa Afya kwa kuwapatia mafunzo katika ubingwa na ubobezi wa utoaji
matibabu mbalimbali. Makamu wa Rais pia amesisitiza kushirikiana katika masuala
ya utamaduni, michezo na lugha ya Kiswahili.
Kwa upande wake Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania Mhe. Eunju Ahn
amesema katika kipindi atakachohudumu nafasi ya Ubalozi nchini Tanzania,
atahakikisha anasimamia na kuharakisha kukamilika kwa makubaliano mbalimbali
yaliyofikiwa baina ya Tanzania na Jamhuri ya Korea ikiwemo ushirikiano katika
madini ya kimkakati na maendeleo ya uchumi wa buluu.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
19 Februari 2025
Ikulu – Chamwino