Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeleta mageuzi makubwa katika sekta ya michezo kupitia uwekezaji wa kimkakati kwenye miundombinu, sera, na ushirikiano wa kimataifa.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Neema Msitha, alieleza hayo alipokutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, akibainisha hatua mbalimbali zilizochukuliwa ili kuimarisha sekta hiyo katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya sasa.
Katika juhudi za kuimarisha sekta ya michezo, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu kwa lengo la kuboresha mazingira ya mazoezi na mashindano. Baadhi ya miradi mikubwa iliyotekelezwa ambayo ni Ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa gharama ya shilingi Bilioni 31, ikiwa ni sehemu ya maboresho ya viwanja vya kimataifa nchini.
Ujenzi wa Uwanja Mpya wa Michezo Arusha ambao unatarajiwa kugharimu shilingi Bilioni 338 hadi kukamilika kwake na Ujenzi wa Uwanja wa Michezo Dodoma, mradi unaotarajiwa kugharimu shilingi Bilioni 310, na ujenzi wake utaanza hivi karibuni.
Serikali pia inaboreshaViwanja vya Mazoezi kama Gymkhana, Leaders Club, TIRDO, Law School, na Uwanja wa Farasi, ambapo jumla ya shilingi Bilioni 21 zimetengwa kwa ukarabati na maendeleo ya viwanja hivyo.
Katibu mtendaji huyo amesema Ili kuhakikisha michezo inakua na kupata maendeleo endelevu, Serikali imefanya maboresho muhimu katika sera na sheria zinazosimamia sekta hiyo. Mabadiliko hayo ni pamoja na Kuondoa Kodi ya Nyasi Bandia, hatua ambayo imerahisisha ujenzi wa viwanja vingi vya michezo katika ngazi ya halmashauri, hivyo kuongeza ushiriki wa vijana katika michezo.
Amesema serikali imeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Michezo, wenye jukumu la kusaidia timu za Taifa, kutoa mafunzo kwa wataalamu wa michezo, kuendeleza vipaji, na kuboresha miundombinu ya michezo nchini.
Pia Mfumo wa Usajili wa Klabu Kidijitali, ambao umeongeza idadi ya vyama vya michezo vilivyosajiliwa kutoka 368 hadi 1,638 ndani ya miaka minne, hatua inayorahisisha usimamizi wa mashindano na klabu.
Akielezea Mafanikio ya Tanzania Katika Mashindano ya Kimataifa amesema Tanzania imeendelea kufanya vyema katika mashindano mbalimbali ya kimataifa, ikiwa ni matokeo ya uwekezaji mkubwa uliofanywa katika sekta ya michezo. Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na:
Ameongeza kuwa katika Mashindano ya Kombe la Dunia – Tanzania ilishiriki Kombe la Dunia la Mpira wa Miguu kwa Watu Wenye Ulemavu na Kombe la Dunia la Mpira wa Miguu kwa Wasichana chini ya miaka 17 nchini India mwaka 2022.
Michezo mingine ni pamoja na Mchezo wa Gofu – Timu ya Taifa ya wanawake ilishinda mashindano ya All Africa Challenge Trophy mwaka 2022, Mchezo wa Riadha – Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mashindano ya vijana wa Afrika Mashariki chini ya miaka 18 na 21 (EARR), ambapo timu ya Tanzania ilimaliza katika nafasi ya pili na ya tatu.
Mashindano ya Kriketi – Tanzania ilishinda ICC Mens T20 World Cup Sub Regional Africa Qualifier na Mens ICC U19 World Cup Qualifier Africa Division 2 mwaka 2024.
Katika Michezo ya Walemavu – Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, hasa katika tenisi ya viti mwendo na mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu.
Msitha amesema Kwa kutambua umuhimu wa kushirikiana na wadau wa kimataifa, Tanzania ilihudhuria Mkutano Mkuu wa Kanda ya Nne wa Kupinga Dawa na Mbinu Haramu Michezoni, uliofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Novemba 2024.
Katibu Mtendaji wa BMT, Neema Msitha, amesisitiza kuwa mafanikio haya yote ni matokeo ya uongozi thabiti wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuweka mazingira mazuri ya kuendeleza michezo nchini.
“Serikali imejipanga kuendeleza mafanikio haya kwa kuwekeza zaidi katika sekta ya michezo ili kuhakikisha Tanzania inazidi kung’ara kimataifa,” alisema Msitha.
Amesema kwa uwekezaji mkubwa katika miundombinu, sera, na ushirikiano wa kimataifa, Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa mataifa yanayopiga hatua kubwa katika sekta ya michezo barani Afrika. Serikali imeahidi kuendelea kuweka mazingira bora zaidi kwa wanamichezo ili kuimarisha zaidi maendeleo ya sekta hiyo.