Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda akizungumza kwenye uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Damas Ndumbaro Jijini Mwanza

Huda ya msaada wa kisheria ikiendelea kutolewa kwa wananchi



Baadhi ya wananchi wakiwa kwenye uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia
………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Damas Ndumbaro amezindua Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia “Mama Samia Legal Aid Campaign” ambayo itafanyika kwa siku 10 Jijini Mwanza.
Uzinduzi huo umefanyika Jumanne 18, 2025 katika viwanja vya Furahisha Wilaya ya Ilemela Mkoani hapa.
Kampeni hiyo yenye kauli mbiu isemayo “msaada wa kisheria kwa haki,usawa,amani na maendeleo” itasaidia kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu masuala ya haki.
Akisoma hotuba kwaniaba ya Waziri Ndumbaro Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema Kampeni hiyo itasaidia kupunguza migogoro iliyopo kwenye jamii.
Aidha, amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi ili waweze kutatuliwa changamoto zao sanjari na kupata elimu itakayowasaidia kuelewa mambo mbalimbali ya kisheria
“Wananchi wanaoishi pembezoni watakuwa wamefikiwa na huduma hii na hawatapoteza muda mwingi katika kushughulikia changamoto zao”, amesema
Kwa upande wake mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Alfred Dede amesema katika kampeni hiyo elimu kuhusu masuala ya kisheria na utawala bora itatolewa kwa umma.
“Elimu kuhusu mapambano ya ukatili ya kijinsia usimamizi wa mirathi na urithi haki za ardhi utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala haki za binadamu na wajibu yakiwemo masuala muhimu katika ndoa yatafundishwa ili jamii iwe na uelewa wakutosha katika masuala hayo”, amesema
Naye Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Angeline Mabula amewaomba watanzania wajifunze kuandika wosia kwani kwakufanya hivyo itasaidia kupunguza migogoro kwenye familia husika.
Awali akizungumza kwenye uzinduzi huo Mwenyekiti wa Msaada wa Kisheria Mkoa wa Mwanza, Yasin Ally amesema kwa mwaka 2024 jumla ya mashauri 172,301 yalisajiliwa na kushughulikiwa kwa njia ya mtandao katika Mahakama za mwanzo huku mashauri zaidi ya elfu 70 yakishughulikiwa kwa njia ya mtandao katika Mahakama za wilaya na Mahakama kuu.