Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea kutoka kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknoloji, Profesa Adolf Mkenda kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tuzo ya kutambua mchango Rais katika kukuza na kuendeleza Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini.
Tukio hilo lilifanyika katika Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 20 ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Februari 17, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kimkabidhi Rais Mstaafu Jakaya Kikwete tuzo ya kutambua mchango wake katika kukuza na kuendeleza Bodi ya Mikopo wa Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini. Tukio hilo katika Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 20 ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Februari 17, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza katika Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 20 ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Februari 17, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete akizungumza katika Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 20 ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Februari 17, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akishuhudia utiaji saini wa ushirikiano wa kikazi katika utoaji na urejeshaji mikopo kati ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini na Taasisi ya Utoaji Mikopo kwa Wanafunzi nchini Korea ya Kusini. Pichani, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Dkt. Bill Kiwia (kushoto) na Bw. Gun Lee, Meneja wa Idara ya Mawasiliano kwa Umma kutoka Korea ya Kusini wakibadilisha nyaraka baada ya utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano huo kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius nyerere jijini Dar es salaam, Februari 17, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………….
*Asema Serikali ilifuta tozo za kulinda thamani ya fedha ili kuondoa changamoto katika urejeshaji wa mikopo.
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imetumia shilingi trilioni 8.2 kugharamia wanafunzi tangu ilipoanzishwa.
Amesema kuwa pia katika kipindi hicho wanafunzi takribani 830,000 wamenufaika na mfumo huo wa ugharimiaji wa elimu ya juu kupitia Bodi ya mikopo.
Amesema hayo leo Jumatatu (Februari 17, 2025) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, iliyofanyika kwenye Kituo cha Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
“Mafanikio tuliyonayo leo, ni matokeo ya utashi wa kisiasa, uongozi thabiti, maono na michango ya viongozi wetu. Viongozi wetu katika awamu zote walifanya kazi kubwa ya kuhakikisha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inafanya vizuri, viongozi wetu walioona mbali kuanzisha mfumo huu wa ugharimiaji wa elimu ya juu kupitia Bodi ya mikopo”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imefanikiwa kukusanya fedha kiasi cha shilingi trilioni 1.5 “Ninatambua marejesho hayo yamepatikana kutokana na jitihada na ubunifu mkubwa ambao unasaidia kuwafikia wanufaika ambao wamehitimu na mikopo yao imeiva”.
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu haiwi mzigo kwa Wanafunzi, Serikali iliamua kufuta tozo za kulinda thamani ya fedha ili kuondoa changamoto katika urejeshaji wa mikopo. “Kwa sasa mnufaika anarejesha kiasi kile kile ambacho amekopeshwa kwani tozo hizo zilikuwa zinasababisha ongezeko la madeni ya mikopo hiyo.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Bodi ya Mikopo kuendelea kuweka mikakati ya kuendana na kasi ya mababiliko ya teknolojia na ifanye maboresho ya kujiunganisha na kuzungumza lugha moja na taasisi za fedha nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa wakati Rais Dkt. Samia anaingia madarakani alikuta fedha zinazotolewa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ilikuwa ni shilingi bilioni 464. “Lakini alipoingia aliagiza fedha kwa ajili ya mikopo ziongezwe, na tuliongeza hadi kufikia bilioni 570, tukaendelea hadi bilioni 654 na sasa ni shilingi bilioni 731”
Ameongeza kuwa Rais Dkt. Samia katika kuhakikisha kada za Sayansi zinaendelea kupewa kipaumbele ili kuzalisha wataalam wengi zaidi, aliiagiza Wizara ya Elimu kutenga fedha kwa ajili ya kuanza kutoa ufadhili kwa ajili ya kada hizo ambayo tuliita Samia Scholarship.
“Wakati tunaanza tulitoa shilingi bilioni 3 kama majaribio, baadae tulitoa bilioni 6 na sasa hivi tumetoa shilingi bilioni 8.9”.
Kwa upande wake, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Kikwete amesema kuwa katika kipindi cha miaka 20, viongozi katika awamu zote wamefanya kazi kubwa katika kuhakikisha bodi ya mikopo inajiongezea uwezo ili kuwahudumia vijana wengi zaidi wa Kitanzania.
“Niliyoyaona na kuyasikia yamenifurahisha sana, uongozi ni kazi ya kupokezana kijiti, mwenzako anakimbia mpaka hapa, wewe unapokea unakimbia mpaka pale, nilikabidhiwa na Mzee Mkapa nikafanya nilichoweza, tukaachia awamu ya tano ikafanya ilichokiweza na ikaiachia awamu ya sita na sasa mambo mazuri zaidi kazi iendelee”
kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu- Athari chanya, Ubunifu na Huduma’’.