Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ametembelea eneo la mradi wa ujenzi unaoendelea kwenye viwanja vya Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ethiopia.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajia kujenga majengo ya Ubalozi yenye Jengo la Ofisi, Makazi ya Balozi, Makazi ya Watumishi wa Ubalozi na Majengo mengine muhimu yatakayokidhi mahitaji ya sasa na ya baadae ya Ubalozi huo.
Eneo la mradi lina ukubwa wa mita za mraba 3,414 ambapo Mkandarasi ameanza kazi ya ujenzi kwenye eneo la mradi.
Ujenzi wa viwanja hivyo utakuwa na faida kwani Serikali itapunguza matumizi ya gharama za kulipa kodi na kuwaweka watumishi katika mazingira bora ya kazi.
Wakati huohuo, Mhe. Waziri Kombo amefanya kikao na ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaohudhuria vikao vya kilele vya Mkutano wa 38 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali utakaofanyika tarehe 15 na 16 Februari, 2025.
Kikao hicho pamoja na masuala mengine kilijadili maandalizi ya jumla ya mkutano huo ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha ushiriki wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unakuwa wenye tija na kufikia lengo lililokusudiwa.