*Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kuadhimisha miaka 20 Februari 17, 2025
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amewataka wahitimu wa vyuo vikuu walionufaika na mikopo inayotolewa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo ili kutoa fursa kwa wanafunzi wengine kunufaika.
Akizungumza leo Februari 13, 2025, ofisini kwake Ilala Boma, Jijini Dar es Salaam, RC Chalamila amesema Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu inatarajia kuadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake. Sherehe hizo zitafanyika Februari 17, 2025, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
RC Chalamila amesema tangu kuanzishwa kwake, Bodi hiyo imewanufaisha zaidi ya wahitimu 830,000 kwa kuwapatia mikopo, hivyo ni muhimu kwa walionufaika kufanya marejesho, hasa wale walioko kwenye ajira rasmi na waliojiajiri.
Aidha, RC Chalamila amepongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kutoka Shilingi bilioni 570 mwaka wa fedha 2021/2022 hadi Shilingi bilioni 787 mwaka wa fedha 2024/2025. Amebainisha kuwa, kwa mwaka huu pekee, zaidi ya wanafunzi 247,000 wananufaika na mikopo hiyo, hatua inayoongeza fursa kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Kuhusu maadhimisho hayo, RC Chalamila amesema kuwa yalianza Februari 10, 2025, kwa maonesho ya huduma za Bodi yaliyofanyika katika mikoa saba ya kikanda: Dodoma, Mwanza, Arusha, Mbeya, Dar es Salaam, Mtwara, na Zanzibar. Maonesho hayo yamepangwa kumalizika Februari 14, yakilenga kuimarisha utoaji wa huduma za Bodi.
Vilevile, RC Chalamila amesema kuwa Februari 15, 2025, kutakuwa na mbio za pole (jogging) zitakazoongozwa na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, kuanzia viwanja vya Farasi, Oysterbay. Kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika Februari 17, 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, ambapo wageni kutoka mataifa mbalimbali barani Asia, Amerika Kusini, Ulaya, na Afrika wanatarajiwa kuhudhuria.